Precision Air yaanzisha safari Dar– Iringa kuanzia Machi 2025

By Imani Nathaniel , Nipashe
Published at 04:50 PM Jan 30 2025
Mkurugenzi Mtendaji wa Precision Air, Patrick Mwanri.
Picha: Mtandao
Mkurugenzi Mtendaji wa Precision Air, Patrick Mwanri.

Katika juhudi za kuboresha huduma za usafiri wa anga nchini, Shirika la Ndege la Precision Air limeanzisha safari mpya za ndege kati ya Dar es Salaam na Iringa, ambazo zitaanza rasmi Machi 03, 2025.

Safari hizi zitaendeshwa mara tatu kwa wiki—Jumatatu, Jumatano, na Ijumaa—zikiunganisha abiria kati ya Dar es Salaam, Dodoma, Iringa, na maeneo mengine kupitia mtandao wa Precision Air na washirika wake.

Akizungumza wakati wa kutangaza huduma hiyo mpya, Mkurugenzi Mtendaji wa Precision Air, Patrick Mwanri, alisema shirika limejipanga kutoa safari za uhakika kwa bei nafuu, huku likizingatia mahitaji ya abiria na maendeleo ya nchi.

"Tunajivunia kuanzisha safari za ndege kwenda Iringa, eneo lenye fursa kubwa za ukuaji wa kiuchumi. Precision Air imejidhatiti kutoa huduma za usafiri wa anga zenye uhakika na kwa gharama nafuu kwa Watanzania wote," alisema Mwanri.

Aliongeza kuwa safari hii mpya ni sehemu ya juhudi za kuimarisha muunganisho wa jamii na kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii nchini. Pia, huduma hii inakwenda sambamba na mkakati wa serikali wa kuendeleza sekta ya utalii, hasa katika Nyanda za Juu Kusini.

"Safari hizi zitawarahisishia watalii kufika Hifadhi ya Taifa ya Ruaha na maeneo mengine yenye vivutio vya utalii mkoani Iringa," alieleza Mwanri.

Zaidi ya kuwa msaada kwa wakazi wa kawaida, huduma hii mpya itasaidia pia kukuza biashara na utalii katika mkoa wa Iringa, ambao unajulikana kwa utajiri wake wa kitamaduni, mandhari ya kuvutia, na sekta ya kilimo. Abiria sasa wataweza kusafiri kwa urahisi kati ya Dodoma, Dar es Salaam, na Iringa, huku wakipata fursa ya kuunganisha safari zao kwa kupitia mtandao wa Precision Air na washirika wake.

Tiketi za safari mpya za Precision Air kuelekea Iringa zinapatikana kupitia tovuti rasmi ya shirika.

Precision Air Services Plc ni shirika binafsi la ndege linaloongoza nchini Tanzania, likitoa safari za ndani na za kikanda katika vituo 13 kote Afrika Mashariki. Shirika hili limejikita katika kuhakikisha usalama, uhakika, na huduma bora kwa wateja wake. Mbali na safari za abiria, Precision Air pia inatoa huduma za matengenezo ya ndege na mafunzo ya sekta ya anga kwa wataalamu wa fani mbalimbali.