Mawaziri wa nishati EAC kujadili uzalishaji umeme

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 12:13 PM Jan 27 2025
Mawaziri wa nishati EAC kujadili uzalishaji umeme.
Picha: Mpigapicha Wetu
Mawaziri wa nishati EAC kujadili uzalishaji umeme.

MAWAZIRI kutoka nchi mbalimbali za Jumuiya ya Afrika Mashariki na watumiaji wakubwa wa nishati wanatarajia kukutana Jijini Arusha katika Mkutano wa Ushirikiano wa Nishati wa Afrika Mashariki (EA-ECS), unatarajiwa kufanyika Januari 29-30 jijini humo.

Mkutano huo utajikita kufungua fursa kwa sekta binafsi, kuhimiza kuwepo kwa mseto wa nishati mbalimbali ili kudumisha ustahimilivu wa gridi ya taifa ili kusaidia ukuaji mkubwa wa viwanda, pamoja na uzalishaji wa umeme kwa matumizi ya kibiashara na biashara za viwandani.

Akizungumzia mkutano huo jana, Andrea Malueth, Naibu Katibu Mkuu (Sekta ya Miundombinu, Uzalishaji, Jamii na Siasa), Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, alisema kwa kuzingatia mafanikio ya mwaka jana, mkutano huo utakuza ushirikiano kote Afrika Mashariki.

Alisema kuwa mkutano huo pia utaangazia dira ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ya ushirikiano wa kina wa kikanda na jukumu muhimu la kukuza viwanda na ushirikiano miongoni mwa wadau.

Alisema mkutano huo utawakutanaisha wazalishaji nishati binafsi Afrika na wadau wa Uhandisi, Manunuzi, Ujenzi, na Fedha (EPCF) kutathimini uwezekano wa uwekezaji na uvumbuzi ulioanzishwa na kampuni muhimu kimkakati, ikijumuisha Vituo vya Data vya Afrika na iXAfrica.

"Kiini cha ukuaji huu wa kikanda wa shughuli za uwekezaji ni Sekretarieti ya Afrika Mashariki (EAC), ambayo inawakutanisha wawekezaji na watengeneza sera pamoja na EnergyNet, kujikita katika "Utajiri wa Rasilimali. Upatikanaji wa Nishati. Fursa za Uwekezaji." alisema na kuongeza kuwa;

“Nishati ni nguzo ya maendeleo na ukuaji na ni muhimu kwa utendaji kazi wa uchumi wa Nchi Wanachama wa Afrika Mashariki.Mkutano wa Ushirikiano wa Nishati wa Afrika Mashariki utatumika kama jukwaa bora la kuendeleza miradi na kuleta mabadiliko yanayoonekana katika sekta hiyo,” alisema

Aliongeza kuwa EA-ECS itakaribisha wanasiasa na viongozi mashuhuri kutoka nchi zote za Afrika Mashariki na sekta zake za nishati katika mkutano huo, ambapo wataungana na wakuzaji biashara wa sekta binafsi ambao wanatengeneza mustakabali wa mazingira ya nishati ya Afrika Mashariki, wakihudumia takriban watu milioni 500.

Kwa upande wa Mtaarishaji wa EnergNet, Elisa Palmioli alisema; "Miaka 10 kutoka sasa, tabaka la kati la watu wa Afrika Mashariki litakuwa na uthabiti zaidi wa kazi, fursa zaidi, na kipato zaidi ukilinganisha na hapo awali. Reli mpya, viwanda, bandari na utalii vitalifanya eneo hili kuwa kivutio kikuu cha uwekezaji duniani, na kujitwalia nafasi hiyo kutoka eneo la Asia na Amerika Kusini,"

Alitaja mafanikio yaliyopatikana kuwa ni pamoja na njia kuu ya umeme ya Ethiopia-Kenya, jambo ambalo linasisitiza uwezekano wa mageuzi wa ushirikiano wa kuvuka mpaka kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Alitaja mafanikio mengine kuwa ni watumiaji wa nje kuongeza hitaji la uzalishaji wa nishati ambapo mkutano huo utazingatia sekta ya madini na miundombinu ya kidijitali.

Mwaka wa 2024, kufuatia Mkutano wa Powering Africa wa EnergyNet huko Washington DC, USA, Mara Holdings iliadhimia nia yake ya kuwekeza Afrika Mashariki kwa kutia saini makubaliano makubwa na serikali ya Kenya, kuonyesha mwelekeo wa kile ambacho kinaweza kubadilisha mwenendo kwa eneo na uhalali wa kibiashara kwa Wazalishaji Nishati Binafsi (IPP).