Bunge: Tumeona kasoro nyingi miradi ya halmashauri, CAG nenda kapekue

By Augusta Njoji , Nipashe
Published at 08:02 AM Feb 15 2025
news
Picha: Mtandao
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere.

BUNGE limeazimia Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kufanya ukaguzi wa kina katika miradi yote yenye changamoto kwenye halmashauri ambayo imejengwa na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) na kubainisha iwapo kuna thamani ya fedha.

Pia limeagiza CAG akague kwa kina miradi ya ujenzi wa majengo ya utawala katika Halmashauri za Wilaya ya Kiteto na Kibiti na Halmashauri ya Mji Ifakara kutokana na kubainika kufanyika malipo kwa kazi ambazo hazijatekelezwa na makandarasi kinyume cha Sheria na Kanuni za Fedha za Umma.

Akiwasilisha jana taarifa ya mwaka ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Halima Mdee, alisema kamati imebaini ucheleweshaji katika kutekeleza miradi ya maendeleo na kusababisha miradi kutokamilika kwa wakati.

Alisema miradi kutokamilika kwa wakati uliopangwa kunachelewesha kupatikana faida ya miradi hiyo kinyume cha dhamira ya serikali.

“Bunge linaazimia serikali ihakikishe inakamilisha miradi yote viporo kabla ya kuanza utekelezaji miradi mipya ili lengo la uanzishwaji miradi hiyo lifikiwe, na CAG afanye ukaguzi wa kina katika miradi yote yenye changamoto ambayo imejengwa na TBA na kubainisha iwapo kuna thamani ya fedha," alisema.

Awali Mdee alisema Halmashauri ya Kilosa iliingia mkataba na Mkandarasi TBA kwa ajili ya ujenzi wa jengo la utawala la halmashauri kwa gharama ya Sh. bilioni 3.7 na mradi huo ulianza kutekelezwa Agosti 2023 na ulitarajiwa kukamilika tarehe 10 Agosti 2026.

Hata hivyo, alisema hadi halmashauri inafika kutoa maelezo mbele ya kamati, utekelezaji mradi huo ulikuwa umesimama na Sh. bilioni moja sawa na asilimia 26 zilikuwa zimeshalipwa na utekelezaji mradi ulifikia asilimia 22.6.

Alisema mradi mwingine ni ujenzi wa Hospitali ya Wilaya katika Halmashauri ya Mji Ifakara ambao Mkandarasi (TBA) mpaka muda ambao kamati inakutana, malipo yalishafanyika kwa asilimia 100, lakini mradi ulikuwa umekamilika kwa wastani wa asilimia 65 kwa majengo yote.

"Dosari iliyobainika katika mradi huu ni fedha zote kutumika na majengo kutokamilika kwa wakati uliopangwa na halmashauri bado inahitaji Sh. milioni 342.9 kukamilisha mradi huu,”alisema.

Pia alisema kuwa katika mradi wa ujenzi wa jengo la utawala la Halmashauri ya Mji Ifakara wenye thamani ya Sh. bilioni 7.4, muda wa zabuni uliisha pasi na mradi kukamilika na Mkandarasi TBA alishalipwa Sh. bilioni 4.2.

"Halmashauri iliingia mkataba mwingine na TBA wenye thamani ya Sh. bilioni 4.5, zabuni hii ilifanyika kwa kazi ambazo hazikufanyika katika zabuni ya kwanza ambayo muda wake uliisha pasipo mradi kukamilika na Mkandarasi ameshalipwa Sh. milioni 502.4 na kufanya jumla ya fedha iliyolipwa kwa mkandarasi kwa zabuni zote mbili kuwa ni Sh. bilioni 4.7.

"Mradi huu ulianza kutekelezwa tarehe 3 Juni, 2018 na ulipaswa kutekelezwa kwa miaka mitatu hadi tarehe 3 Juni 2021. Licha ya kiasi tajwa hapo juu kulipwa kwa mkandarsi ambayo ni sawa na asilimia 64 ya gharama yote ya mradi, mradi umetekelezwa kwa asilimia 47 tu," alisema.

Mwenyekiti huyo alisema dosari zilizobainika katika utekelezaji ujenzi wa jengo la utawala ni mkandarasi kulipwa zaidi ya kiwango cha utekelezaji mradi kinyume cha sheria katika hati ya malipo Na.4 kwa kiasi cha Sh. milioni 189.5. Sh.milioni 63.1 zimesharejeshwa na kubakiwa na deni la Sh. milioni 126.3 kiasi ambacho hakijarejeshwa hadi sasa.

Alisema miradi iliyotekelezwa na Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko – Mkandarasi (TBA) wa jengo la ofisi ya utawala la halmashauri kwa gharama ya Sh. bilioni 3.3, changamoto ni kutokurejeshwa kwa malipo yaliyozidi kazi zilizofanyika Sh. milioni  237.4.

"Kuhusu Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti, katika mradi wa ujenzi wa jengo la utawala la halmashauri – gharama ya mradi Sh. bilioni 5.3 iliingia makubaliano na Mkandarasi SUMA JKT na mshauri elekezi wa mradi huu ni Aru Built Environment Consulting Company Ltd (ABECC)," alisema.

Mwenyekiti huyo alisema kutokana na kusuasua kwa utekelezaji wa mradi huo, hadi kamati inakutana na Ofisa Masuuli wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti, mradi huo umetekelezwa kwa asilimia 82 na jumla ya Sh. bilioni 4.01 sawa na asilimia 75 za gharama za mradi zimekwishatumika.

Mdee alisema kamati imebaini kuwapo ukiukwaji taratibu za malipo ambapo baada ya kukamilika kwa awamu ya kwanza ya mradi, Mkandarasi SUMA JKT alimwandikia msimamizi wa mradi ABECC ili kubadili njia za malipo kutoka ‘Certificate’ kwenda kwenye utaratibu wa malipo wa ‘milestone'.

Halmashauri iliridhia mabadiliko hayo ya malipo kinyume cha taratibu. Kwa muktadha huo, halmashauri ilipokea Sh. milioni 389.1 kutoka Hazina na kuzilipa kwa Mkandarasi Suma JKT kwa utaratibu wa milestone (yaani halmashauri inanunua vifaa na mkandarasi analipwa gharama za ufundi pekee).

Katika ujenzi wa jengo la utawala la Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa, mwenyekiti huyo alisema makandarasi ni TBA na SUMA JKT. Awamu ya kwanza mkandarasi alikuwa TBA na gharama ilikuwa Sh. milioni 649.6 na awamu ya pili mkandarasi alikuwa SUMA JKT na gharama Sh. bilioni 2.89.

Alisema hadi kamati inakutana na Ofisa Masuuli, mradi ulikuwa umesimama na Sh. bilioni 3.83 zimeshalipwa. Kamati ilibaini fedha za mradi Sh. milioni 390.9 zilitumika kwa matumizi yasiyokusudiwa na Sh. milioni 500 zimerudishwa Hazina kutokana na kuchelewa kutumika kwenye mradi.

Pia Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro, katika Mradi wa ujenzi wa jengo la utawala la halmashauri, mkandarasi ni TBA na gharama za mradi ni Sh. bilioni 3.1.

Kutokana na kuchelewa kutekelezwa kwa mradi, kulisababisha kuongezeka kwa gharama za mradi kwa Sh. milioni 371.9 na hivyo kufanya mradi kuwa na gharama ya Sh. bilioni 3.5.

TARATIBU ZAKIUKWA

Mdee alisema kamati imebaini baadhi ya halmashauri kukiuka taratibu za malipo kwa kazi ambazo hazijatekelezwa na makandarasi kinyume cha Sheria na Kanuni za Fedha za Umma.

"Dosari hiyo imebainika katika Halmashauri za Wilaya za Kiteto na Kibiti na Halmashauri ya Mji Ifakara ambapo kiasi kikubwa cha fedha kimelipwa kwa miradi ambayo haijatekelezwa kinyume cha utaratibu," alisema.

Mdee alisema taarifa ya CAG imebainisha changamoto za malipo yanayofanyika kwa makandarasi ambazo ni kutozingatiwa kwa taratibu za malipo ikiwa ni pamoja na makandarasi kulipwa kabla ya utekelezaji mradi.

"Kukiukwa kwa taratibu za malipo kumesababisha miradi kutotekelezwa kwa wakati. Bunge linaazimia serikali (Wizara ya Fedha) ihakikishe inachukua hatua za haraka juu ya taratibu za malipo zilizofanywa kwa makandarasi waliotekeleza miradi ya ujenzi wa majengo ya utawala ya halmashauri katika Halmashauri za Wilaya za Kiteto na Kibiti na Halmashauri ya Mji Ifakara," alisema.