Biteko: Uchumi wa Bluu unategemea utunzaji mazingira, viumbe bahari

By Mary Geofrey , Nipashe
Published at 09:10 AM Jul 05 2024
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko.
Picha: Mpigapicha Wetu
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko.

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko, amewataka Watanzania kulinda viumbe vya baharini na kuhifadhi mazingira yake kwaajili ya vizazi vilivyopo na vijavyo

Dk. Biteko amesema hayo jana wakati akifungua kongamano la Tatu la Uchumi wa Bluu mwaka 2024, yenye kaulimbiu: 'Kuunganisha Usalama Baharini, Utunzaji wa Mazingira na Maendeleo ya Teknolojia kwaajili ya Ukuzaji wa Uchumi wa Buluu'

“Tunapofanya majadiliano leo (jana), tujikite kwenye kanuni uendelevu, usawa na uvumbuzi ili hatimaye kongamano hili liwe mwanga unaotuongoza kwenye uchumi wa buluu unaoinua jamii zetu, ninawasihi kila mmoja wenu ashiriki kikamilifu ili tuweze kupata matokeo chanya ya kongamano hili,” ameema Dk. Biteko.

Dk. Biteko amesema pia uchumi wa bluu huchochea uvumbuzi wa fursa  kama vile teknolojia ya kibayoteknolojia na nishati ya bahari, kutoa suluhu za nishati mbadala na tiba, inasaidia juhudi za kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi kupitia ulinzi wa mifumo ikolojia, na kuhakikisha  Ulinzi na usalama wa bahari, ambao ni muhimu kwa usalama wa usafiri wa majini na kuzuia shughuli haramu baharini. 

"Pamoja na mazuri yote hayo, uchumi wa bluu unakabiliwa na changamoto kadhaa ikiwa ni pamoja na uvuvi wa kupita kiasi, uchafuzi wa bahari, mabadiliko ya hali ya hewa, uvuvi haramu, uharibifu wa makazi na kutopatikana kwa taarifa sahihi. Kama ilivyo katika nchi nyingine duniani, Tanzania pia inakabiliwa na changamoto hizo," ameisisitiza Dk. Biteko.

Naye Waziri wa Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa, amesema uchumi wa bluu ni uchumi mtambuka unaohusisha sekta mbalimbali amesema kongamano hilo limekua chachu katika kutoa fursa na mafunzo kwa Watanzania katika sekta ya bahari.