Asilimia 40 watumishi wa serikali ni 'mizigo'

By Romana Mallya , Nipashe
Published at 08:06 AM Feb 15 2025
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene.
Picha: Mtandao
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene.

SERIKALI imesema takriban asilimia 40 ya watumishi wa umma hawafanyia kazi kutokana na miongoni mwao kuwa wavivu, wazembe, wagonjwa na wale ambao viongozi katika taasisi zao hawataki wafanye kazi bali wamekaa tu.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene, aliyasema   hayo jana jijini hapa, wakati akifunga Kikao Kazi cha Tano cha siku yatu cha Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA). 

Simbachawene alisema kila aliyeajiriwa serikalini amepewa majukumu ya kufanya kazi lakini utafiti uliofanywa na Tume ya Utumishi wa Umma umebainisha nguvu kazi hiyo haitumiki sawasawa.

“Utafiti umeeleza na kuangalia sababu na serikali kupata hasara. Kwa sababu mtu anapokuja katika taasisi yako analipwa mshahara na serikali, hivyo kazi yako ni kuhakikisha kila kunapokucha kila mtumishi wa umma anafanya kazi.

 “Ziko taasisi na baadhi ya watumishi ambao ni wavivu. Ukiwachukua wavivu na  wale wagonjwa  tayari ni karibu asilimia 25 hadi 30 ya nguvu kazi haifanyi kazi kwa siku. Wako ambao wanafika katika taasisi zetu na ninyi hamuwapi kazi kwa sababu mnajiuliza na kujihoji  ‘amekujaje huyu, kaletwa na nani.

 “Kama ana CV (wasifu)  nzito ndiyo kabisa analeta tishio katika taasisi anawekwa benchi hafanyi kazi, ‘eti huyu tutamkomesha mpaka atakapoondoka mwenyewe’,” alisema.

 Waziri alisema kwa hiyo wakijumlisha na wavivu, wazembe , wagonjwa na ambao viongozi katika taasisi hawataki wafanye kazi wanafikia asilimia 40.

 “Nitumie kikao hiki kusisitiza hapa kuna Ma-MD (Wakurugenzi), CEO (Watendaji Wakuu) na RAS (makatibu Tawala wa Mikoa)  ambao ndio husimamia rasilimali watu.

 “ Wizara yangu kazi yake ni msimamizi mkuu wa watumishi wa umma kwa nia ya kutoa huduma kwa wananchi ikiwamo teknolojia ya habari na mawasiliano  katika kuboresha huduma kwa haraka na stahiki.

 “Lakini, bado yako majukumu nisisitize, ufanisi wa matumizi sahihi ya nguvu kazi katika taifa. Kazi ya maofisa rasilimaliwatu katika taasisi wanawawakilisha nyie viongozi wakuu ni kuhakikisha walioajiriwa serikalini wanafanya kazi sawasawa,” alisema.

Simbachawene alisema serikali inapoajiri watu wamepewa majukumu ndiyo maana wanaanza na kama, hivyo kama hawafanyi kazi maana yake mtendaji mkuu unapata hasara katika taasisi yako.

“Humkomoi yule anachukua mshahara wa bure. Niwaombe hakikisheni rasilimaliwatu inafanya kazi ipasavyo. Isitokee mtu wakati mwingine na CEO tunapokuletea mtu dhamira yetu inaweza ikawa si unayoitaka wewe. Tunataka hata kupunguzapunguza nguvu zako inaweza ikawa hauendi sawa tukakubadilishia hawa tukakuletea hawa,” alisema.

Simbachawene pia alionya tabia ya baadhi ya viongozi kutotengeneza watu wa kurithi  nafasi zao  baada ya kustaafu na kusema ni sababu ya taasisi kuyumba kwa sababu ya kukosa utaratibu wa kuwaandaa wengine kuchukua majukumu.

Alisema kutokana na kuwapo kwa tabia hiyo, wale wenye uwezo mzuri wanashughulikiwa katika taasisi na wenye mtindo huo wanatoka na kutamba kuwa wamebaki wenyewe.  

Aliwakumbusha watu hao kwamba kuna siku watastaafu na wakumbuke wao ni binadamu lolote linaweza kutokea. 

“Ili tujenge nchi yenye hadhi na heshima, lazima watu wafanye kazi, turuhusu wenye vipaji kujitokeza. Kama wenye vipaji watakuwa wanashughulikiwa hakika nchi itapata hasara wakati hivi sasa inaheshimika,” alisema.

 Waziri aliwaeleza viongozi wa taasisi za umma pamoja na watumishi ambao wanashindwa kutekeleza agizo la Rais Samia Suluhu Hassan kuhusu matumizi Mfumo wa  E-Mrejesho, kuchukuliwa hatua.

 Alisema Rais ameagiza umuhimu wa matumizi ya teknolojia ya Habari na mawasiliano (TEHAMA) katika kuboresha utendaji kazi wao na utoaji wa huduma kwa umma.

 Simbachawene alisema Rais ambaye katika uzinduzi wa kikao kazi hicho aliwakilishwa na Makamu wa Rais, Dk. Philip Mpango, aliiagiza ofisi yake kusimamia vyema matumizi ya mfumo wa e-Mrejesho na kuhakikisha taasisi zote za umma zinautumia katika kukusanya kero za wananchi zinazowasilishwa. 

 “Nitumie nafasi hii, kuwakumbusha viongozi wa taasisi za umma, pamoja na watumishi kutekeleza agizo hili la Rais, nasi kama wizara tutachukua hatua kwa wale watakaokaidi agizo hili.

“Vilevile, wizara inazielekeza taasisi za umma, ambazo bado hazijahuisha taratibu za utendaji kazi wake (Business processes), kuhakikisha zinaandaliwa na kuwekwa kwenye maandishi, ili iwe rahisi kujenga mifumo inayowasiliana na kubadilishana taarifa kwa urahisi zaidi,”aliagiza.

 Waziri Simbachawene alitoa rai kwa taasisi zote za umma ambazo bado zina kiwango kidogo cha utekelezaji wa Serikali Mtandao, ziongeze kasi ya  matumizi ya TEHAMA katika utekelezaji wa majukumu yao na kuishirikisha Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA), ili kwa pamoja tutimize malengo yetu ya kuijenga Serikali ya Kidijitali.

Alisema serikali imedhamiria kuimarisha na kuongeza matumizi TEHAMA ili kwenda sambamba na maendeleo ya sayansi na teknolojia kwa kuwa shughuli nyingi duniani zikiwamo za kiuchumi kwa sasa zinafanyika kwa kutumia teknolojia hiyo.

 Alisema wizara kupitia e-GA, imejipanga kupanua wigo wa upatikanaji wa huduma mtandao kwa umma kidijitali sambamba na kuboresha upatikanaji wa mawasiliano ya simu nchi nzima, ili kuwawezesha Watanzania kupata huduma kwa wakati na kwa gharama kupitia mifumo ya TEHAMA.