Zuchu anazidi kufoka, Diamond hana habari

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 08:29 AM Jan 19 2025
Mwanamuziki maarufu wa Bongo Fleva, Zuchu.
Picha: Mtandao
Mwanamuziki maarufu wa Bongo Fleva, Zuchu.

WAKATI mwanamuziki maarufu wa Bongo Fleva, Zuchu, amezidi kuonesha hasira zake kwa kutishia kuwaburuza mahakamani watangazaji wa Wasafi, bosi na mpenzi wake Diamond Platnumz, ameonekana kuziba masikio na kuendelea na mambo yake.

Juzi Zuchu aliandika waraka mrefu akilalamikia vitendo ambavyo vinamchafua na kuwatuhumu watangazaji wa redio kuwa nyuma ya vitendo hivyo, hivyo anafikiria kuchukua hatua za kisheria.

Katika hatua nyingine, Zuchu aliondoa utambulisho wake wa lebo ya WCB, katika ukurasa wake wa Instagram, jambo linaloashiria kuwa anaweza kujitoa kusimamiwa na lebo hiyo wakati wowote.

Zuchu amekuwa katika mgogoro na mtangazaji Juma Lokole, kila mara na safari hii hali imekuwa mbaya kiasi ambacho msanii huyo ameonekana kushindwa kuvumilia.

Hata hivyo, Mkurugenzi wa Wasafi Media, Diamond Platnumz, ambaye pia ana uhusiano naye wa kimapenzi, yuko kimya na sakata hilo, huku akionekana yuko bize kutangaza shoo yake katika mtandao wa Netflix.