Zanzibar yaeleza utekelezaji wa Ilani ya CCM 2020-2025

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 09:45 AM Jan 19 2025

Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla.
Picha: CCM
Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla.

Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla, amewasilisha muhtasari wa mafanikio ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kipindi cha 2020-2025, akieleza hatua kubwa zilizopigwa katika sekta mbalimbali, zikiwemo uchumi na elimu.

Mafanikio ya Kiuchumi

Kwa mujibu wa Hemed, Zanzibar imeshuhudia ukuaji wa uchumi kutoka asilimia 5.1 mwaka 2021 hadi asilimia 7.5 mwaka 2024. 

Aidha, Pato la Taifa limepanda kutoka shilingi trilioni 4.2 mwaka 2020 hadi trilioni 6.288 mwaka 2024, jambo linaloashiria maendeleo makubwa katika ustawi wa taifa.

Maendeleo ya Elimu

Sekta ya elimu imepiga hatua kubwa, ambapo bajeti ya Wizara ya Elimu imeongezeka kutoka shilingi bilioni 265.5 mwaka wa fedha 2021/2022 hadi bilioni 830 mwaka 2024/2025, sawa na ongezeko la asilimia 212.6. 

Serikali imefanikiwa kujenga shule mpya 116 zenye jumla ya madarasa 2,713, ikiwemo shule 35 za ghorofa.

Pia, ufaulu wa wanafunzi wa kidato cha nne umeongezeka kutoka asilimia 55.4 mwaka 2020 hadi asilimia 85.6 mwaka 2023, huku ufaulu wa kidato cha sita ukifikia asilimia 99.9 mwaka 2024.

Hemed ametoa taarifa hiyo leo, Januari 19, 2025, wakati wa Mkutano Mkuu Maalumu wa CCM unaoendelea katika Kituo cha Mikutano cha Jakaya Kikwete, jijini Dodoma.