MAKAMU Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Stephen Wasira, ametaja kazi mbili alizo nazo kuwa ni kushinda uchaguzi na kukamata dola ya Muungano na Zanzibar.
Amesema ili kukamata dola ni lazima kupata kura na zinakuja kwa kutimiza miradi ambazo tayari CCM imejenga miundombinu ya barabara, elimu, afya, maji na miradi ya kimkakati.
Akizungumza baada ya kuchaguliwa, Wasira alisema hakuna kitu hata kikienda sawa kikakosa manung’uniko na kwamba uchaguzi wa serikali za mitaa ulifanyika vizuri na kazi iliyopo ni kukamata dola.
“Kura zinapigwa kwa kutekeleza ahadi na hivi sasa tunakwenda kupiga kura. Tumejenga zahanati na shule kila mahali, tumewatua ndoo kinamama kichwani kila mahali. Miradi ya kitaifa tuliyoambiwa baada ya Rais (John) Magufuli kufariki dunia akakabidhiwa Samia na sasa ni SGR hadi Dodoma, kuna daraja la Busisi linakamilika, Bwawa la umeme linakamilika sasa tushindwe kwasababu gani?” alihoji
Alisema sababu za kushinda, nia na uwezo wanao na huo ni wito wake na ameanza tayari kazi.
“Alisema dunia na wana CCM wajue kuwa CCM ni chama cha umoja, amani na maendeleo na kwamba wanapewa nchi kwa sababu ya kuendeleza maridhiano na amani na hayaji kwa kuzungumza na mtu mmoja bali ni kuridhiana na jamii.
“Wadau wote tutashirikiana nao katika amani kwa kuwa ni msingi wa maendeleo na asanteni kwa kunipa heshima hii, kazi na iendelee,”alisema.
Awali, alishukuru vikao vya chama kwa kumwamini kwa kuwa mambo yenyewe ni magumu na si rahisi.
“Mambo ni magumu na wala si rahisi. Unaambiwa njoo leo leo mimi ndiyo nimejua wakati Kamati Kuu inakutana sikujua mnamzungumza nani, mi nilikuwa nimejikalia huko nakunywa chai na wengine, NEC (Halmashauri Kuu ya Taifa) mimi ni mjumbe nikaenda nikasema kumbe mlikuwa mnanizungumza mimi,”alisema.
Alisema Rais Samia anajua kuweka siri watu wanashangaa walikuwa na makamu wanafikia saba lakini yeye amemtoa mmoja.
“Mimi ni nani kati ya wote watu ni wengi mno. CCM ina hazina ya watu wazee wapo wengi sana lakini Mungu amesema wewe. Namshukuru Mungu kwa kukuongoza na kwa imani yako sikutambua leo (jana) naijua siku nyingi kwamba una imani na mambo ninayofanyia chama chetu lakini Mungu alikuwa hajakuongoza, lakini imekutana na nguvu ya mwenyewe,”alisema.
Alisema alifurahi jina lake kupelekwa kwenye mkutano mkuu kwa kuwa nusu ya wajumbe amezungumza nao kwa simu kwa kipindi cha miaka 20 iliyopita.
“Nawashukuru hata wale saba kuwa na mashaka maana ni mara ya kwanza nitakapoifanya najua watapungua,”alisema.
KURA ZA KISHINDO
Akitangaza matokeo ya uchaguzi, Spika wa Bunge Dk. Tulia Ackson, alisema Wasira ameshinda kwa kura 1910 sawa na asilimia 99.42.
Alisema wajumbe waliopiga kura ni 1921 na kura nne ziliharibika hivyo kura halali 1917 na kati ya hizo kura za hapana ni saba za ndiyo ni 1910.
NENO LA KINANA
Kinana alisema CCM ni chama imara, kikubwa na kinaheshimiwa na Watanzania na kimepewa dhamana ya uongozi wa nchi na hana shaka hata kidogo kitaendelea kupewa dhamana hiyo kwa sababu kina sera na ilani nzuri na kuwajali na kuwasikiliza wananchi.
Alisema Mwenyekiti huyo alimpendekeza mara mbili kuwa Makamu ambayo ni Aprili 2021 na Desemba 2022 na kumshukuru kwa heshima aliyompa na ataendelea kuienzi maisha yake yote.
“Kama kuna sifa zozote ambazo nimezipata ndani ya chama si zangu ni za wana CCM wote kwa sababu chama chetu si chama cha viongozi ni chama cha wanachama. Bila msaada wa wana CCM bila uongozi na imani ya viongozi nisingeweza kutimiza wajibu wangu kama nilivyofanya. Nilijitahidi kadiri ya uwezo wangu nilifanikiwa kwa kiwango fulani,”alisema.
Aliwaomba wana CCM kumuunga mkono Rais Samia na kwamba wanampenda wanamheshimu na watathamini kazi kubwa anayofanya ya kujituma na kujitolea na kutekeleza ilani.
“Sina shaka hata kidogo katika uchaguzi ujao wana CCM watakupendekeza na watanzania watakuchagua ili tuendelee kupata maendeleo makubwa zaidi, nimpongeze Rais Hussein Mwinyi kwa kazi anayoifanya Zanzibar amekuwa mbunifu wa miradi mbalimbali na anafanya kazi kwa ufanisi,”alisema.
Aliahidi kuwa alipoandikiwa barua na Rais ya kuendelea kushirikiana na wana CCM katika kufanya kazi ya chama, atatimiza ahadi hiyo.
“Nimpongeze Wasira kwa kuchaguliwa nimepata nafasi ya kufanya kazi na Wasira ndani ya chama ni mtu hodari, mchapakazi, mwadilifu na mzalendo kwa taifa lake. Nina hakika nafasi ya Makamu Mwenyekiti iko salama chini ya uongozi wa Wasira,” alisema.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED