‘Siri mafanikio NSSF ni uwekezaji sekta binafsi’

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 07:36 AM Jul 05 2024
MKURUGENZI Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Masha Mshomba.
Picha: Mpigapicha Wetu
MKURUGENZI Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Masha Mshomba.

MKURUGENZI Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Masha Mshomba amefichua siri ya mafanikio ya NSSF kuwa yamechangiwa na serikali inavyohamasisha wawekezaji katika sekta binafsi, kuweka mazingira mazuri na kuwezesha kupata waajiri na wanachama wengi wapya katika sekta binafsi.

Mshomba alisema hayo alipotembelea banda la NSSF baada ya ufunguzi wa Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (DITF), maarufu Sabasaba yaliyobeba kaulimbiu: "Tanzania Sehemu Sahihi kwa Biashara na Uwekezaji." Maonesho hayo yamefunguliwa na Rais wa Jamhuri ya Msumbiji, Filipe Nyusi, akisindikizwa na mwenyeji wake, Dk. Samia Suluhu Hassan.

Akizungumza na waandishi wa habari katika banda la NSSF, Mshomba alisema kwa mujibu wa taarifa za hesabu ambazo hazijakaguliwa katika mwaka wa fedha 2023/2024, thamani ya NSSF kwa sasa inafikia trilioni 8.5 sawa na ongezeko la asilimia 77 ikilinganishwa na miaka mitatu iliyopita.

“Ongezeko hili ni kubwa hasa ukizingatia kuwa ndani ya miaka mitatu iliyopita ukuaji wa NSSF umekuwa mkubwa mno, hivyo tunampongeza sana Rais Dk. Samia kwa juhudi anazoweka kuhakikisha mazingira ya biashara hapa nchini yanakuwa mazuri ambayo yamechangia mafanikio haya,” alisema Mshomba.

Aidha, alisema wakati NSSF inaendelea kutekeleza mpango wake wa maendeleo unaoishia Juni 30, 2026, wanatarajia thamani ya Mfuko kufikia trilioni 11 ambayo itakuwa ni zaidi ya mara mbili ikilinganishwa na kipindi Rais Dk. Samia alipoingia madarakani.

Mshomba alisema kwa sasa NSSF imeelekeza nguvu ya kuwafikia wanachama wapya waliopo katika sekta isiyo rasmi ili waweze kujiunga na kuchangia katika NSSF kwa kuwa tayari wameshaweka mifumo mizuri ya usajili na uchangiaji pamoja na mafao yanayovutia kupitia Mpango wa Kitaifa wa Sekta Isiyo Rasmi.

Kuhusu ushiriki wa NSSF katika maonesho hayo, alisema ni kwa ajili ya kutoa elimu ya hifadhi ya jamii kwa wanachama na wadau kuhusu huduma mbalimbali inazotoa mfuko huo zikiwamo usajili wanachama kutoka sekta binafsi na sekta isiyo rasmi, uchangiaji, kulipa mafao, uwekezaji pamoja na uhakiki wa wastaafu.

Mshomba amesema pia wanatumia maonesho hayo kuwaeleza wanachama mambo makubwa ambayo NSSF imeyafanya kupitia huduma za TEHAMA na sasa wanachama wanaweza kujisajili kupitia lango la huduma binafsi kwa mwanachama na lango binafsi kwa mwajiri.

Alisema NSSF inaendelea kupata ushirikiano mkubwa kutoka serikalini na wataendelea kuboresha huduma zao mbalimbali.