WIZARA ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, juzi iliwasilisha bungeni makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha wa 2024/25 ambayo yameainisha miradi mbalimbali itakayotekelezwa na lengo kubwa ni kuongeza ufanisi.
Jerry Silaa, Waziri wa Wizara hiyo, wakati akiwasilisha hotuba ya makadirio hayo, alibainisha kuwa ili kutekeleza majukumu hayo kwa ufanisi, aliomba bunge kuidhinisha Sh. 171,372,508,000.
Fedha hizo, alisema ni kwa ajili ya kutekeleza vipaumbele mbalimbali ikiwamo kuimarisha mifumo ya utatuzi wa migogoro ya ardhi na kasi ya upangaji, upimaji na umilikishaji ardhi. Vingine ni kuimarisha mifumo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika utunzaji kumbukumbu, upatikanaji wa taarifa za ardhi, kuhakikisha kunakuwapo na nyumba bora, ukuaji wa sekta ya miliki na kuimarisha mipaka ya kimataifa.
Aidha, alisema katika mwaka unaomalizika, wizara imetekeleza kwa mafanikio masuala mbalimbali ikiwamo utatuzi wa migogoro ya ardhi huku akibainisha kwamba imechukua hatua dhidi ya watumishi waliokengeuka kimaadili wakiwamo 22 waliosimamishwa kazi kupisha uchunguzi wa tuhuma zinazowakabili, huku saba walifukuzwa kazi na wawili wakipewa onyo.
Kuhusu mafanikio, alisema miradi iliyosimama kwa muda mrefu, ukiwamo wa Kawe 711, sasa inaendelezwa. Mradi huo, alisema kwa sasa umefikia asilimia 35 na unatarajiwa kukamilika Aprili, 2026 ukiwa na thamani ya Sh. bilioni 169.
Katika kushughulikia migogoro ya ardhi iliyoonekana kuwa kero kitaifa, alisema wizara kwa mwaka wa fedha 2023/2024 imetatua migogoro 4,565 kupitia kliniki tembezi za ardhi nchi nzima. Pia alisema wizara imeongezewa bajeti Sh. bilioni 287.66 ili kulipa madeni ya wazabuni, watumishi na makandarasi.
Pia maombi 191 ya ardhi ya uwekezaji mkubwa, eneo la hekta 11,613 yaliidhinishwa katika mwaka wa fedha 2023/24.
Mafanikio mengine ya wizara hiyo, ni yale yanayohusu wawekezaji wa ndani na nje, ambao thamani yake ni Sh. trilioni 1.08.
Licha ya kuainisha mafanikio hayo, uko ushahidi wa wazi kwamba wizara hiyo hivi karibuni imeonyesha dhamira ya dhati katika kutatua kero zilizokuwa zikiharibu taswira yake na serikali kwa ujumla.
Ziara za viongozi, wakiongozwa na Waziri Silaa ni kielelezo tosha cha kuivalia njuga migogoro ya ardhi ambayo imekuwa ikiripotiwa kila uchao.
Hatua iliyofikiwa na wizara katika kutatua kero hizo ndani ya wizara hasa katika halmashauri mbalimbali ambako watumishi wa sekta ya ardhi wamekuwa wakituhumiwa kuhusika na migogoro hiyo ni ya kupigiwa mfano na kupongezwa.
Ni dhahiri kwamba kama moto uliowashwa mwaka wa fedha unaoelekea ukingoni uliwachoma wengi wakiwamo wale waliokuwa wamedhulumu ardhi za wananchi, utaendelea kwa kasi kubwa zaidi katika mwaka ujao wa fedha. Viongozi wanapaswa kufukua zaidi madudu yaliyojificha pamoja na kusimamia vyema mipango ya matumizi ya ardhi ili kuwe na viwango bora kwenye sekta hiyo.
Pamoja na imani hiyo, uongozi wa juu pekee wa wizara hauwezi kutatua migogoro ndani ya sekta hiyo bali zinahitajika nguvu za pamoja baina ya wizara na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na wizara zingine za kisekta. Wizara hizo ni pamoja na zile zenye dhamana ya maliasili na utalii, kilimo na mifugo kwa kuwa shughuli zao zinahusiana moja kwa moja na masuala ya ardhi.
Aidha, uaminifu kwa maofisa waliopewa dhamana ya kusimamia sekta ya ardhi katika ngazi za halmashauri, unahitajika katika kufikia mafanikio malengo yaliyokusudiwa. Pia elimu itolewe kwa viongozi wa vijiji na wananchi kuhusu namna bora ya matumizi ya ardhi.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED