RAIS Samia Suluhu Hassan juzi alizindua Tume ya Rais ya Kutathmini na Kushauri kuhusu Masuala ya Kodi na kubainisha kuwa mrejesho alioupata katika ukusanyaji wa kodi unaonesha kuwapo kwa malalamiko ya mianya ya ukwepaji wa kodi, makusanyo kidogo, huku mengi yakiingia mifukoni mwa watu.
Hatua hiyo, kwa mujibu wa Rais Samia inasababishwa ma baadhi ya watumishi wa serikali kutokuwa waadilifu na kuwapo kwa utaratibu usioridhisha katika utoaji wa misamaha ya kodi kwa wawekezaji.
Rais alisema pamoja na kuwapo kwa mianya hiyo ya ukwepaji kodi, idadi ya walipakodi ni ndogo kulinganisha na zaidi ya Watanzania milioni 60 kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi. Alisema idadi ya walipakodi ni zaidi ya milioni mbili kati ya watu milioni 66 na kwamba wakitoa watoto na watu wengine ambao hawastahili kulipa kodi, hawapungui milioni 37 ambao wanaweza kulipa kodi.
Pamoja na walipakodi kuwa wachache, Rais alisema serikali imeimarisha mifumo ya ukusanyaji mapato na kuijengea uwezo Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na kuimarisha mazingira ya kufanya biashara, hivyo kuchangia kuleta matokeo chanya kwa makusanyo ya kikodi ambayo yameongezeka kutoka wastani wa Sh. bilioni 850 kwa mwezi mwaka 2015 hadi wastani wa Sh. bilioni mbili kwa mwaka 2023, katika ripoti iliyotolewa hivi karibuni na TRA, kuna mafanikio makubwa baada ya kukusanya mwezi uliopita zaidi ya Sh. trilioni tatu.
Mwasisi wa taifa la Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere, aliwahi kusema nchi yoyote isiyokusanya kodi lazima itakuwa na matatizo yakiwamo ya rushwa. Hivyo ndivyo inavyosadifu kutokana na kauli ya Rais kuhusu kuwapo kwa mianya ya ukwepaji kodi na baadhi ya watumishi wasio waaminifu kuchepusha fedha za umma na kuziingiza katika mifuko yao.
Kutokana na uwapo wa hali hiyo, kuna uwezekano mkubwa hata takwimu zilizotolewa na TRA kuwa makusanyo yamepanda hadi Sh. trilioni tatu zikawa ndogo. Ni dhahiri kwamba kama mianya ya ukwepaji kodi ikazibwa na kuwekwa kwa mazingira rafiki katika ulipaji kodi, kiasi hicho kingepanda hata kufikia zaidi ya Sh. trilioni nne. Kwa mantiki hiyo, kazi kubwa inapaswa kufanyika kwa kuziba mianya hiyo ikiwamo kuchukua hatua dhidi ya baadhi ya watumishi wanaosababisha serikali kukosa mapato kwa sababu mbalimbali.
Katika miaka ya karibuni, kwa mfano, ilishuhudiwa serikali ikitumia vyombo vya dola kama vile polisi wakiwa na bunduki wakienda kudai kodi kwenye sehemu za biashara. Hali hiyo ilisababisha taharuki na kuwafanya baadhi ya wafanyabiashara kufunga shughuli zao na kukimbilia nchi zingine.
Sambamba na kutumia mitutu ya bunduki kudai kodi, baadhi ya maofisa wa TRA kwa kushirikiana na askari polisi walikuwa wakitumia mwanya huo kuwatisha wafanyabiashara na kuwataka wawapatie chochote kitu na waliokuwa wakigoma walikuwa wakitishiwa kufikishwa mahakamani kwa madai ya kukwepa kodi.
Aidha, migomo mbalimbali ya wafanyabiashara katika maeneo kama Dar es Salaam, Arusha, Mwanza ukiwamo ule wa karibuni uliotikisa na kusababisha serikali kukosa mapato, chanzo kikubwa kilikuwa malalamiko ya kubambikiwa kodi. Jambo hilo lilijitokeza pia wakati wa ziara ya Rais mkoani Ruvuma kwamba hata mamalishe na babalishe wamekuwa wanadai TRA wamekuwa wakighasi kwenye shughuli zao.
Kama wahenga wasemavyo yaliyopita si ndwele tugange yajayo, ukurasa mpya unapaswa kufunguliwa ambao utaweka mazingira rafiki kati ya TRA na wafanyabiashara ili makusanyo zaidi yaongezeke. Kuongezeka kwa mapato ya serikali yatokanayo na kodi yataifanya serikali kupunguza mzigo wa kukopa kwa ajili ya matumizi yake na miradi ya maendeleo.
Licha ya kuweka mazingira rafiki, uandaliwe utaratibu kwa TRA kuongeza idadi ya walipakodi kwa kuwasajili ikiwamo wananchi kuwezeshwa kiuchumi kwa kufungua miradi na biashara ambazo zitachangia kuongeza mapato.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED