WATANZANIA wapenda haki na amani Afrika na duniani kote, kesho wataadhimisha Kumbukizi ya Miaka 25 ya kifo cha Rais wa Kwanza na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.
Maadhimisho ya mwaka huu, ambayo yanafanyika sambamba na kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru kwa mwaka 2024, yanafanyika jijini Mwanza na mgeni rasmi atakuwa Rais Samia Suluhu Hassan.
Maadhimisho hayo, kama ambavyo yamekuwa yakifanyika kila mwaka, yalitanguliwa na midahalo na makongamano mbalimbali kujadili masuala anuai yakihusisha fikra, falsafa na mitazamo ambayo aliviishi na kuvitenda wakati wa uhai wake.
Miongoni mwa mambo hayo ni elimu, ukombozi wa Afrika, vita dhidi ya rushwa, utawala bora huku akisisitiza uadilifu kwa viongozi, kutojilimbikizia mali na vitendo vya rushwa.
Kwa ujumla, tangu alipofariki dunia, ni miaka 25 ambayo kwa baadhi ya vijana waliokuwa watoto na waliozaliwa wakati huo au miaka michache baadaye, kwa sasa ni wakubwa ama wameoa au kuolewa lakini fikra, matendo na falsafa zake bado vinaishi na pengine ni muhimu kuliko wakati ule.
Moja ya mambo hayo ni mapambano dhidi ya rushwa. Nyerere alikemea waziwazi vitendo vya rushwa, ikiwamo watu kutoa rushwa, ili kupata huduma au kutumia fedha kupata uongozi.
Alisema waziwazi kwamba mtu anayetumia fedha kupata uongozi, huyo hafai kwa sababu anafanya hivyo kwa manufaa binafsi badala ya wananchi wanaompa kura.
Kwa mantiki hiyo, alihimiza watu wanaotaka uongozi wajichunguze kuhusu usafi wao na maadili. Alisema fedha kisiwe kigezo cha mtu kupata uongozi bali uadilifu.
Jambo lingine alilolisisitiza ni elimu, huku akisisitiza kuwa iwe nguzo ya kumkomboa Mtanzania kifikra, ili kuyatawala mazingira yanayomzunguka, ikiwamo kutatua vikwazo vinavyomkabili yeye na jamii yake.
Kuhusu Muungano, alisisitiza kuwa unapaswa kulindwa kama mboni ya jicho na mtu yeyote atakayediriki kuuchezea, hana budi kushughulikiwa kwa gharama zozote.
Licha ya mambo hayo, Nyerere alikuwa akisisitiza Afrika kuungana na kuwa na nguvu moja, ili kujikomboa kiuchumi baada ya mataifa mengi kupata uhuru kutoka kwa wakoloni.
Katika uongozi wake viwanda vingi vilijengwa, huku akisisitiza matumizi ya bidhaa za ndani zinazotokana na viwanda hivyo. Alisisitiza pia watu kufanya kazi kwa bidii na kutaka wavivu, wazembe na wazururaji wachukuliwe hatua.
Wakati kesho atatimiza miaka 25 tangu alipofariki dunia, mambo aliyoyasisitiza na kuyapiga vita bado yanatendeka. Rushwa bado ipo katika maeneo mbalimbali, ikiwamo baadhi ya watu kutafuta uongozi kwa kutoa rushwa.
Ni vyema katika kumuenzi, Watanzania wakaziishi fikra na falsafa zake, kwa kufanya kazi kwa bidii kama alivyohimiza. Pia viongozi wanapaswa kujiepusha na vitendo vya rushwa na kutenda haki.
Wakati mwaka huu ni wa uchaguzi wa serikali za mitaa, ni vyema Nyerere akaenziwa kwa watu wanaotafuta uongozi kwa rushwa, wakawekwa kando na wananchi kuchagua watu waadilifu. Pia vyama vya siasa katika hatua za mchujo, viwaondoe wale wote wanaoendekeza rushwa katika kusaka uongozi.
Kwa jumla, katika kumuenzi Nyerere, njia pekee ya kufanya hivyo ni kuyaishi matendo yake na kuheshimu fikra na falsafa zake.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED