Wafanyabiashara wanaochoma nyama katika eneo la kwa Mrombo, Kata ya Murieti, mkoani Arusha, wamelalamikia kufanya biashara zao katika mazingira magumu, na licha ya kulipa ushuru, bado eneo hilo halijafanyiwa maboresho kwa muda mrefu.
Akizungumza kwa niaba ya wafanyabiashara wenzake leo Jumapili, Mwijuma Mbaruku, amesema eneo hilo licha ya watu wengi kufika ikiwemo viongozi wa Serikali na watalii, mazingira yake ni hatarishi katika kutoa huduma hiyo, kutokana na uwepo kwa maji machafu yaliyotuama katika eneo hilo.
Amesema kwa miaka mingi eneo hilo halifanyiwi ukarabati wowote licha ya kuchangia fedha za ushuru, hivyo wamemuomba Mkuu wa Mkoa, Paul Makonda, awasaidie ili wafanye biashara zao katika mazingira safi na salama na hivyo kulinda afya za walaji.
"Tunaomba watuwekee mifereji ya kupitisha maji, haya mazingira hayavutii tuna jina kubwa na kila anayefika Arusha lazima aje kula nyama hapa kwa Mrombo, hadi wazungu wanakuja, lakini ukiangalia haya mazingira hayaridhishi, watuboreshee ili wanaokuja wafurahie mazingira," amesema.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED