MWANAFUNZI wa Kidato cha Kwanza katika Shule ya Sekondari Miyandi, wilayani Ikungi, mkoani hapa, Felista Charles (16), aliyezuiwa hospitalini kwa siku saba baada ya kushindwa kulipa deni la Sh. milioni 1.3 ameruhusiwa baada ya Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi kulilipa.
Binti huyo ambaye alilazwa Hospitali Teule ya Makiungu kwa matibabu baada ya kung’atwa na nyoka Machi 21, mwaka huu, aliruhusiwa baada ya afya yake kuimarika lakini kutokana na deni aliendelea kubaki hospitalini hapo.
Mama mzazi wa mwanafunzi huyo, Sisilia Neriko, akizungumza na mwandishi wa habari hizi, amesema waliruhusiwa kutoka hospitalini tangu (Machi 21) baada ya hali ya mgonjwa kuimarika, lakini uongozi wa hospitali hiyo uliwazuia kutoka hadi deni la Sh. 1,350,000 lilipwe.
“Tangu tuliporuhusiwa kutoka tumekaa hospitalini siku saba hivyo tumetoka Machi 28, 2024 baada ya fedha kulipwa. Tunawashukuru viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi na uongozi wa Shule ya Sekondari Miyandi kwa kufanikisha suala hili, Mungu awabariki,” amesema.
Januari 23, mwaka huu, mwanafunzi huyo aling'atwa na nyoka katika mguu wake wakati akilima katika shamba la moja wa walimu shuleni hapo aliyefahamika kwa jina moja la Robert, baada ya kupewa adhabu ya kufanya kazi shambani humo.
Amesema baada ya tukio hilo, walimu wa shule hiyo walimpeleka kwa mganga wa kienyeji anayefahamika kwa jina maarufu la njoka ambaye inaaminika hutibu wagonjwa waliong'atwa na nyoka, lakini alishindwa kutokana na sumu kusambaa na mguu kuvimba.
Neriko amesema baada ya hali mwanafunzi kuwa mbaya ndipo wazazi walijulishwa ambapo baba mzazi, Charles James, alikwenda kwa mganga huyo wa kienyeji kumchukua kwa pikipiki.
Amesema kutokana na hali ya mtoto kuwa mbaya na kushindwa kukaa katika pikipiki, walilazimika kukodi gari la kumpeleka katika Hospitali Teule ya Makiungu.
Amesema mwanafunzi huyo alifikishwa hospitalini hapo Januari 24, mwaka huu, na siku iliyofuata alifanyiwa upasuaji wa mguu kuondoa baadhi ya nyama kwenye mguu ili kuzuia sumu ya nyoka isiendelee kusambaa mwilini.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED