MBUNGE wa Simanjiro (CCM) mkoani Manyara, Christopher Ole Sendeka, amefunguka alivyojinusuru na dereva wake kushambuliwa kwa risasi kuwa ni baada ya kujibu mapigo.
Akisimulia shambulio hilo lilivyotokea juzi ambalo tayari Jeshi la Polisi limepeleka timu ya wataalam wa uchunguzi wa matukio kutoka makao makuu ya polisi, Ole Sendeka alisema kilichomnusuru ni ujasiri wake wa kuamua kuwatisha kwa kujibu mashambulizi.
Shambulio hilo lilitokea juzi saa 12:45 jioni katika Kijiji cha Ngabolo, wilaya ya Kiteto, mkoani Manyara.
“Kulikuwa na gari ambalo lilikuwa linanifuatilia kwa nyuma, tukawapisha kidogo wapite kulia. Walipofika usawa wetu, wakaanza kumimina risasi upande wa dereva na baada ya hapo, wakavuta kwenda mbele halafu wakaanza kuzipiga za usoni.
“Na sisi tukakata kona kugeuza. Na mimi nikaanza kupigapiga (risasi) za juu pale kuwatishiatishia, ndipo tukafanikiwa kugeuza na kuondoka. Walikuwa na silaha kubwa na silaha ndogo. Hakuna aliyepata madhara na tulikuwa mimi na dereva wangu. Ni gari tu ndilo wamelichakaza, wamelipigapiga.
“Hatujazihesabu (risasi) lakini zipo risasi moja, mbili, tatu, nne; kama nne hivi au tano zipo waziwazi (matundu ya risasi yanaonekana kwenye gari),” amesema.
Hata hivyo, Ole Sendeka alipoulizwa kama kuna sababu yoyote anayohisi kwa yeye kushambuliwa kwa risasi, alisema bado hawezi kusema jambo kwa wakati huu na wala si rahisi kujua sura za waliohusika katika tukio hilo.
Katika taarifa kwa umma iliyotolewa jana na Msemaji wa Jeshi la Polisi Nchini, Naibu Kamishna (DCP) David Misime alisema jeshi hilo limepokea taarifa ya Mbunge wa Simanjiro.
Misime amesema tayari jeshi limepeleka timu ya wataalam wa uchunguzi wa matukio yaliyohusisha matumizi ya risasi kutoka Makao Makuu ya Polisi, kuchunguza ili kubaini waliohusika ni kina nani na madhumuni au kusudio lao lilikuwa nini.
Amesisitiza kuwa polisi wanafuatilia tukio hilo kwa ukaribu na baada ya kulichunguza taarifa kamili itatolewa.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED