WIKI hii katika toleo mojawapo la gazeti la Nipashe, kulichapishwa taarifa kwamba katika vijiji vinne katika kata ya Kisiriri, Iramba mkoani Singida, umeibuka mtindo wa watu kutengwa na jamii iwapo watashindwa kulipa faini waliyotozwa kutokana na makosa mbalimbali wanayoyafanya.
Hatua hiyo ambayo imeibua mijadala katika jamii na taharuki kwa wananchi, imeanzishwa baada ya kuibuka kwa vikundi vya kimila, maarufu kama Nkiri. Vikundi hivyo vimeelezwa kuwatoza wananchi wanaofanya makosa kama vile kutoshiriki shughuli za kijamii faini kama vile ng’ombe, mbuzi au fedha. Yeyote anayetozwa faini hiyo kama inavyoamuliwa, anatengwa na jamii ikiwamo kutojumuishwa katika shughuli za kijamii.
Kwa mujibu wa uchunguzi wa Nipashe, vikundi hivyo vina safu za viongozi wanaosimamia utekelezaji wa mila au utamaduni huo na mwananchi asiyetoa faini hiyo, hutengwa na kijiji au kitongoji na haruhusiwi kwenda dukani kununua bidhaa yoyote.
Mwananchi anayeshindwa kulipa faini hiyo kama itakavyoamuriwa, haruhusiwi kwenda kusaga nafaka wala kwenda katika huduma za afya kupata matibabu na hawaruhusiwi kuhudhuria msiba utakapotokea katika eneo anamoishi na atakapofiwa hakuna atakayemfariji na atakayeonekana kafanya hivyo naye anatozwa faini.
Katika kuhakikisha yote hayo yanatekelezwa, vikundi hivyo ambavyo viko kila kijiji na kila kitongoji, vina sheria vilizojiwekea na wanufaika wakubwa wa faini hizo zinazotozwa ni pamoja na viongozi wa maeneo husika. Kuwapo kwa tatizo hilo kumekuwa kero kwa wananchi kwa kuwa hakuna hatua zozote kila wanapotoa taarifa kwa uongozi kutokana na kwamba ni sehemu ya wanufaika.
Mbaya zaidi, vikundi hivyo vimekwenda hatua kubwa zaidi kwa kujiwekea mazingira ya kupata fedha au mifugo kwa faini kwa kuwatuhumu watu kuwa wachawi au wanasababisha vifo vya watu kimiujiza. Watu wanaodaiwa kufanya hivyo, wanatozwa hadi ng’ombe watatu na baadhi ya mifugo hiyo inayotozwa faini inachinjwa na nyama yake kugawiwa kwa wanakijiji wote au wanakitongoji.
Kwa mantiki hiyo, viongozi serikali na wa vikundi hivyo, wanapoona kuna uhitaji wa nyama au fedha, wanatengeneza mazingira ya kuwatuhumu watu kwa makosa na hatimaye kuwapangia faini hizo. Kwa kufanya hivyo, watu wanakamatwa na kudaiwa kuwa ni wachawi au wamehusika na vifo vya watu kwa njia za kishirikina na hatimaye kuwatoza fedha au mifugo.
Jambo la kusikitisha ni kwamba wako baadhi ya wananchi wanaofikishwa katika vyombo vya sheria lakini wanaachiwa baada ya kubainika kuwa hakuna makosa ya kuwatia hatiani. Pamoja na kuachiwa na mahakama, viongozi hao wanang’ang’ania walipe faini vinginevyo watatengwa na jamii.
Suala hili si geni katika jamii mbalimbali za Watanzania kwani limekuwa likifanyika miaka mingi katika mikoa mingi nchini lakini si kwa kumkomoa mtu au kikundi cha watu bali kuwafanya watu wawajibike ndani ya jamii wanayoishi. Mtu anaposhindwa kuhudhuria mkutano wa kitongoji, kijiji au msiba, anafikishwa katika baraza la kusomewa tuhuma zake kisha kumtoza faini iwapo atakiri au kutiwa hatiani kuwa ametenda kosa.
Pamoja na kuwapo huko, kwa namna linavyoendeshwa katika vijiji hivyo linavuka mipaka ya ubinadamu. Mtu atazuiwaje kupata huduma kama vile kununua mahitaji yake dukani au kupata matibabu katika kituo cha afya?
Katika zama hizi za ustaarabu, jambo hilo halipaswi kupewa nafasi katika jamii ya Watanzania kwa sababu linarejesha hali ya kizamani ya ujima ambayo watu wanafikia hatua ya kukomoana. Jambo hilo linaweza kusababisha mauaji na hata ukosefu wa amani ndani ya jamii husika.
Wakati umefika sasa wa viongozi wa serikali kuanzia ngazi ya wilaya hadi mkoa kuchukua hatua kwa kukemea kwa nguvu zote jambo hili pamoja na hatua za kinidhamu na kisheria dhidi ya wale wanaoendekeza tabia hizo. Hatua zinapaswa kuchukuliwa kwa sababu kama imefikia watu wanatuhumiwa kwa mauaji kwa njia za kishirikina, jambo hilo lisipokemewa linaweza kusababisha kushamiri na kuota mizizi kwa ramli chonganishi ambazo hatimaye zitafanya watu kuanza kuchukua sheria mkononi dhidi ya watuhumiwa.
Mila na desturi zilizopitwa na wakati hazina budi kukemewa na kutokomezwa ili kuifanya jamii ya Watanzania, mahali popote, kuishi kwa amani, umoja na mshikamano badala ya uadui na uhasama. Vitendo kama hivyo havina nafasi na visipewe nafasi asilani.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED