MIGOGORO ya ardhi katika maeneo mengi nchini imekuwa chanzo cha vurugu kwa wakulima na wafugaji.
Suala la wakulima na wafugaji kugombea ardhi limekuwa likishamiri katika maeneo mbalimbali nchini huku wakulima wakitaka ardhi ya kulima na wafugaji wakitaka sehemu ya kulishia mifugo yao.
Hali hiyo imesababisha baadhi yao kuingia katika mapigano na hata kusababisha vifo na wengine kubaki na vilema vya kudumu.
Migogoro hii inaweza kutatuliwa kama kukiwa na mipango mizuri kutoka kwa watekelezaji ambao ni mabaraza ya ardhi.
Hata hivyo, kumekuwapo na malalamiko kuwa baadhi ya viongozi wa mabaraza hayo ndio chanzo cha migogoro hiyo huku wakituhumiwa kuhusishwa na suala la rushwa.
Hivi karibuni kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, Dorothy Semu, amekemea kile alichodai "rushwa kwa baadhi ya viongozi katika mabaraza ya ardhi".
Akitoa mfano wa Wilaya ya Kiteto alipokuwa katika mwendelezo wa ziara zinazofanywa na viongozi wakuu wa chama hicho kuwa ni
ni moja ya ‘makao makuu ya migogoro ya ardhi’ ambayo inasababishwa na mgongano kati ya wakulima na wafugaji.
Anaigeukia serikali kwa kutoonesha kwamba migogoro itakwisha kwa kujipanga vizuri na kuongeza kasi kushughulikia matatizo hayo.
Kimsingi kinachotakiwa ni kuwapo kwa mifumo bora ya kutatua changamoto za ardhi na wanaoongoza mabaraza ya ardhi kuwa na elimu ya kutosha ya namna ya kuitatua.
Wananchi wamekuwa wakiingia migogoro ya wenyewe kwa wenyewe kwa kuuziwa ardhi mara mbili mbili kutokana na baadhi ya watendaji kutokuwa na weledi na kuweka mbele maslahi yao binafsi.
Hata hivyo Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Geophrey Pinda, akiwa mkoani Kilimanjaro, alionya watendaji wa ardhi wanaokiuka maadili.
Katika mkutano wake na wananchi, Naibu waziri huyo, amewaonya watendaji hao kutokubali kuwa hawafai kuwa kwenye nafasi zao.
"Nikimwambia Katibu Mkuu huyu utendaji kazi wake unaripotiwa kwamba hafai, tutatuma vyombo vitakuja kukutafakari upya.
"Usikubali dawati lako liwe chanzo cha mgogoro, upelekwe kwa Mkuu wa wilaya, kwa Mkurugenzi, kwa mbunge na jambo lile uliloanzisha wewe linakwenda mpaka kwa Rais. Haiwezekani! Kila mtu ajitafakari."
Upatikanaji wa hatimiliki za ardhi pia umekuwa tatizo kubwa kiasi cha kusababisha wananchi wanaponunua ardhi kuamua kuiendeleza bila kusubiri taratibu.
Ukiritimba na ucheleweshaji kwa sababu tu baadhi ya maofisa kutaka rushwa limekuwa tatizo kubwa.
Naibu Waziri huyo pia alitoa maelekezo kwa Ofisi za Wasajili wa Hati nchini kuharakisha mchakato wa utoaji hatimiliki za ardhi ili wananchi waweze kunufaika nazo ikiwa ni pamoja na kuaminiwa kupata mikopo katika taasisi za kifedha.
Ameliagiza dawati la usajili lisilaze kazi kwa kutoa hati ili ziende kwa wananchi.
Kadhalika maofisa ardhi wanaojihusisha na ugawaji kiwanja kimoja mara mbili wameonywa na kwamba wizara yake itachukua hatua kali za kinidhamu dhidi ya mtumishi yeyote atakayekiuka maadili ya utumishi wa umma kwa taaluma yake.
Kwa mujibu wa Naibu waziri, Ofisa yeyote atakayehusishwa kwenye jambo la kugawa kiwanja kimoja mara mbili, atachukuliwa hatua kali.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED