SERIKALI imekuwa ikisisitiza kuongezwa kwa kasi ya uwekezaji kwa lengo la kukuza uchumi na kutoa ajira kwa vijana wa Tanzania. Msisitizo huo umeleta matokeo chanya kutokana na kampuni mbalimbali za kigeni kuingia nchini na kuwekeza kwa kujenga viwanda na kufungua biashara za bidhaa kutoka mataifa mbalimbali.
Mbali na kuwapo kwa kampuni na wafanyabiashara kutoka nje ya nchi, pia kumekuwa na wazawa wanaoibuka kwa kuanzisha viwanda na biashara kubwa sambamba na wale wanaoagiza bidhaa kutoka mataifa ya nje na kuuza katika maeneo mbalimbali nchini.
Katika kuhakikisha biashara na uwekezaji vimekuwa na manufaa, taasisi za utoaji vibali kwa ajili ya uwekezaji na sheria zilizokuwa vikwazo pamoja na tozo utitiri vilivyokuwa vikilalamikiwa na wafanyabiashara vimeondolewa. Huduma zote kama vile usajili, vibali vya uwekezaji, masuala ya kodi sasa zinatolewa katika sehemu moja tofauti na ilivyokuwa mwanzo.
Kwa ujumla, kumekuwa na kufurika kwa bidhaa za ndani na za nje katika miji mbalimbali ikiwamo mikubwa kama vile Dar es Salaam, Arusha, Mwanza, Dodoma na Mbeya.
Bidhaa za kila aina zinapatikana takribani miji yote mikubwa na midogo Tanzania, hivyo kuibuliwa kwa ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja miongoni mwa vijana wa Tanzania. Kwa mantiki hiyo, umaskini wa kipato miongoni mwa vijana wa Kitanzania na hivyo mzunguko wa fedha mitaani kwa kiasi fulani umeanza kuonekana.
Pamoja na mafanikio hayo, kumekuwa na malalamiko kutoka kwa baadhi ya wazawa kwamba wanaoitwa wawekezaji au wafanyabisahra wakubwa kutoka nje ya nchi kama vile China, wanafanya kazi au biashara ambazo wanapaswa kufanya wafanyabiashara wadogo tena wazawa.
Hivyo ndivyo ambavyo imekuwa ikisisitizwa na serikali kwamba wageni wanaokuja nchini wasiruhusiwe kufanya kazi ndogo zinazoweza kufanywa na wazawa. Hata kwa kada za wataalaamu kuna sheria ambayo inakataza kada mbalimbali ambazo zinaweza kufanywa na Watanzania kutofanywa na raia wa kigeni.
Pamoja na msisitizo huo, hali imekuwa tofauti kwa sababu wako hata maofisa wa ngazi za chini kutoka nje wanafanya kazi ambazo Watanzania wengi wana uwezo na sifa za kuzifanya. Inashangaza kuona hata wahasibu na maofisa wa taaluma mbalimbali wanaingia na kufanya kazi ambazo wako vijana wengi wa Kitanzania ambao wana uwezo na ujuzi wa kuzifanya.
Katika sekta ya biashara, kwa mfano, imekuwa ikisisitizwa kuwa wafanyabiashara wa nje wanaoingia nchini, wanatakiwa kufanya biashara za jumla kwa kuwauzia wafanyabiashara wadogo. Kinyume chake, wako wafanyabiashara wa kigeni wanaouza bidhaa za rejareja kama wale wadogo jambo ambalo limekuwa likilalamikiwa na wafanyabiashara wengi.
Katika eneo la Kariakoo, Dar es Salaam, kwa mfano, kuna raia wa mataifa mbalimbali, wakiwamo kutoka China ambao wana maduka ya bidhaa za jumla na rejereja huku maofisa wa serikali waliopewa jukumu la kusimamia sheria za biashara na uwekezaji wakiwa kimya.
Jambo hilo limesababisha migogoro baina ya wafanyabiashara hao wa kigeni na wazawa kiasi cha baadhi ya matukio kurushwa katika mitandao ya kijamii. Mbali na migogoro hiyo, kuwapo kwa watu kama hao kutoka nje, kunatishia kudumaa kiuchumi kwa wafanyabiashara wadogo na wa kati wa Tanzania.
Ni vyema jambo hilo likaangaliwa kwa jicho la kipekee kabla ya kusababisha madhara kwa wazawa. Kama kuna sheria zinazosimamia masuala ya biashara na uwekezaji zitekelezwe na kama kuna ulegevu, zipewe meno zaidi ili zing’ate.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED