Jamii itafakari na kuchukua hatua ongezeko mauaji, ukatili

Nipashe Jumapili
Published at 02:16 PM Dec 22 2024
Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Anthony Mtaka
Picha: Mtandao
Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Anthony Mtaka

KWA muda mrefu sasa kumekuwa na taarifa za kuwapo kwa mauaji kwenye mikoa mbalimbali sambamba na ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto. Baadhi ya sababu zinazotajwa kuwa chanzo cha vitendo hivyo ni wivu wa kimapenzi, tofauti kati ya wanandoa na tamaa ya kupata utajiri.

Sababu nyingine inayotajwa ni imani za kishirikina hasa zinazochangia  mauaji ya wazee na vikongwe kwamba wanahusika na vifo vya wanafamilia. Katika baadhi ya makabila, imekuwa kawaida kuwa kikongwe au mzee anapokuwa na macho mekundu, anadaiwa kuwa ni mchawi, hivyo hana budi kuuawa kwa kuwa kuendelea kuishi kwake anaweza kusababisha vifo vya watoto na vijana katika eneo husika. 

Vitendo hivyo, kwa ujumla, vimekuwa vikishamiri siku hadi siku huku vyombo vya habari vikitangaza matukio hayo yanayotokea kila kona ya nchi.  Kutokana na kukithiri huko, wadau mbalimbali wakiwamo viongozi wa serikalli, wa dini na wanaharakati, wamekuwa wakikemea huku wakitaka hatua zaidi zichukuliwe dhidi ya watu watakaobainika kujihusisha na mauaji hayo pamoja na ukatili. 

Hali hiyo imesababisha viongozi wa dini hasa maaskofu wakati wa sikukuu kama vile Krismasi, Pasaka, Maulidi na Iddi pamoja na makongamano mbalimbali, wamekuwa wakipaza sauti kutaka hatua zichukuliwe kwa kuwa matukio hayo yanaharibu taswira njema ya taifa iliyojengeka kwa miaka mingi. 

Aidha kila mwaka kumekuwa na siku 16 za kupinga ukatili, ikiwa ni sehemu ya kutoa elimu kuhusu madhara ya ukatili na mauaji ya watu wasio na hatia kama vile vikongwe, wanawake na watoto. Pamoja na jitihada zote hizo, bado vitendo hivyo vinaendelea kushamiri na kuota mizizi ndani ya jamii. 

Hatua hiyo pia imemwibua Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Anthony Mtaka, ambaye juzi alikuja juu na kuhoji kukithiri kwa matukio ya mauaji, ukatili dhidi ya wanawake na watoto mkoani humo kama yanatokana na matatizo ya afya ya akili au ushetani.

Mtaka alitoa kauli hiyo kwenye kikao na makundi mbalimbali kichofanyika mjini Njombe  kujadili jinsi ya kukabiliana na matukio hayo katika jamii, baada ya kuelezwa takwimu za matukio hayo na kuweka bayana kwamba yanachafua sura ya mkoa ambao umekuwa maarufu kwa uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara. 

Bila kuuma maneno, Mtaka alisema matukio hayo pia yanaondoa ubinadamu na kufedhehesha utu wa mtu na haki katika jamii, hivyo hayavumiliki na hayapaswi kuendelea kutokea ndani ya mkoa huo. Alisema kutokana na kuenea kwa vitendo hivyo, jamii inapaswa kujiuliza chanzo chake ni nini na utamaduni huo unatoka wapi na ni jamii gani inayokusudiwa kujengwa kwa mustakabali wa taifa siku zijazo.

Mkuu huyo wa mkoa alikiri wazi kwamba kwa mtazamo wake, anadhani serikali haijafanya juhudi za kutosha katika suala hilo, hivyo kuna haja ya kufanya mambo makubwa zaidi kukomesha. Pia alishauri jamii na kila mmoja kwenye nafasi yake ya uongozi au mazingira, kuzungumza kwa uzito mkubwa jambo hilo kutokana na athari zake kwa jamii na taifa kwa ujumla. 

Aidha, kutokana na sababu alizosema kama tatizo ni afya ya akili, viongozi wa dini wanapaswa kuhubiri katika nyumba za ibada kwa kuhimiza waumini wao wakapimwe na kupatiwa ushauri wa kisaikolojia. Pia aliwakumbusha viongozi wa siasa kulizungumzia suala hilo kwa undani na kuchukua hatua zinazostahili. 

Kama alivyosema Mtaka, kuna umuhimu mkubwa wa kila mtu kusimama katika nafasi yake kukomesha vitendo hivyo kwa sababu vina athari kubwa kiuchumi na kijamii. Wakati suala la uwekezaji na maendeleo ya viwanda likipewa kipaumbele, kuendelea kwa vitendo hivyo kunaweza kukwamisha wawekezaji kuweka mitaji yao, hivyo kusababisha taifa kushindwa kutimiza azma yake.