MARA kwa mara, madaktari wakiwamo mabigwa na wabobezi pamoja na wataalamu wa lishe, wamekuwa wakitoa ushauri kuhusu namna ya ulaji bora ili kujiepusha na maradhi hasa magonjwa yasiyo ya kuambukiza.
Katika kufanya hivyo, pia wamekuwa wakisisitiza vyakula bora kwa wajawazito na watoto ili kujikinga na madhara mbalimbali ikiwamo udumavu kwa watoto.
Hatua hiyo ya madaktari na wataalamu wa lishe inatokana na kasi kubwa inayoendelea sasa ya watu kupatwa na maradhi yasiyo ya kuambukiza kama vile kisukari, saratani, shinikizo la juu la damu na maradhi ya moyo. Maradhi hayo kwa sasa ndiyo yamekuwa tishio kubwa kwa afya za watu wengi na yamekuwa chanzo kikubwa kwa vifo vya maelfu ya watu hasa katika nchi zinazoendelea, Tanzania ikiwamo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), Dk. Mohammed Janabi, kwa mfano, amekuwa akihimiza namna watu wanavyotakiwa kula huku akihimiza watu kupunguza ulaji wa baadhi ya vyakula kama vile nyama nyekundu, vyakula vya wanga mafuta na sukari pamoja na unywaji wa pombe huku akisisitiza kwamba ni hatari kwa afya. Pamoja na msisitizo huo, baadhi ya watu wamekuwa wakibeza na hata kukejeli kuwa wanapokula vyakula hivyo na kunywa pombe, wanachangia pato la taifa.
Kama wahenga wasemavyo mzaha mzaha hutumbuka usaha, ndivyo inavyokuwa kwa sababu kuendelea kupuuza ushauri huo wa madaktari, ndivyo hatari inavyozidi kwa kuwa idadi ya watu wanaougua magonjwa hayo inaongezeka. Sababu kubwa ni kupuuza ushauri huo hata ule wa watu kutakiwa kufanya mazoezi.
Wakati hayo yakiendelea kwa wataalamu kuhimiza ulaji bora wa vyakula na kuepuka baadhi ya vyakula ili kupambana na maradhi, limeibuka tishio lingine kuhusu mfumo wa ulaji vyakula. Kwa mujibu wa Bingwa wa Upasuaji na Mkuu wa Idara ya Upasuaji Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) Mloganzila, Dk. Eric Muhumba, watu wanaokaa muda mrefu bila kula, wako hatarini kupata vidonda vya tumbo (ulcers).
Kadhalika, anasema watu wanaokula mlo kupitiliza bila kuzingatia lishe, wamo hatarini kuingia kwenye kundi la walio na unene uliopindukia (obesity). Kwa mujibu wa Dk. Muhumba, Unene uliopindukia kitaalamu hutokea wakati fahirisi ya uzito wa mwili (body mass index) wa mtu ni 30 au zaidi.
Mtaalamu huyo anasema kundi la watu wanaoshinda njaa muda mrefu, wamo hatarini kupata vidonda vya tumbo, kutokana na aside (tindikali) iliyomo tumboni na kwamba sababu kuu ya vidonda vya tumbo ni asidi nyingi tumboni ambayo inazalishwa unaizalisha wewe mwenyewe. Sababu ya kuwa na vidonda ni maambukizi ya bakteria wanaoitwa Helicobacter pylori (H. Pylori).
Aidha, kwa mujibu wa mtaalamu huyo, hatari ya aside inayozalishwa kwa wingi tumboni hutokana na mtu kutokula muda mrefu, kula vyakula vinavyozalisha kemikali hiyo pamoja na msongo wa mawazo, huweza kusababisha utumbo kutoboka na kuhitajika upasuaji wa dharura. Pia anasema mtu kukaa na njaa muda mrefu, kunasababisha acid inakuwa yenyewe tumboni inaanza kula kuta za tumbo.
Taarifa hii ya mtaalamu huyo bingwa wa afya, inapaswa kuzingatiwa kwa watu kufuata utaratribu bora wa ulaji wa vyakula badala ya kupuuza na kuona ni jambo la mzaha. Wako watu ambao muda mwingi wamekuwa hawali vyakula, pengine siku nzima huku wakisema wanaweka miili yao sawa bila kujua wanahatarisha afya zao pamoja na kufupisha maisha yao.
Wataalamu wa maandiko matakatifu wanasema Mwenyezi Mungu hutumia watu tofauti kuwakumbusha wanadamu kuishi maisha mema, hivyo ni dhahiri kwamba kauli za madaktari kuhusu masuala ya afya ni mwendelezo huo na watu wanatakiwa kuyafuata ili kujiepusha na maradhi yanayoweza kukatisha uhai wao.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED