RAIS Samia Suluhu Hassan juzi aliwaapisha viongozi kadhaa aliowateua hivi karibuni kwa ajili ya kuanza utekelezaji wa majukumu mapya waliyopangiwa. Viongozi hao ni mawaziri, naibu mawaziri, katibu mkuu wa wizara na makatibu tawala.
Katika hotuba yake baada ya kuwaapisha wateule hao, alitoa maelekezo kwa kila mmoja kuhusu nini anachopaswa kufanya kulingana na nafasi yake. Pamoja na maelekezo hayo, Rais aliwasisitiza viongozi hao kuwa wanapaswa kutambua kwamba nafasi za uongozi walizo nazo si za kudumu bali ni za muda huku akifananisha na koti la kuazima kuwa anayempa anaweza kumvua wakati wowote anatavyoona inafaa.
Rais pia aliwaambia viongozi hao waache kujineemesha kwa kutumia nafasi zao bali watambue kuwa wamepewa nafasi hizo kwa ajili ya kuwatumikia wananchi. Alisisitiza kwamba hatakuwa na mswalie mtume kwa wale wote watakaoshindwa kutimiza majukumu yao kwa ufanisi na weledi huku wakifuata sheria, kanuni na taratibu.
Kubwa zaidi, aliwakumbusha kuwa hawana budi kuzingatia viapo walivyokula vya kuwa waadilifu kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mujibu wa Katiba pamoja na kutokutoa siri za serikali isipokuwa ama katika kutekeleza majukumu yao au watakavyoagizwa na Rais.
Pia aliwasisitiza kuwa wanapaswa kuheshimu viapo hivyo kwa sababu wameapa huku wakiwa wameshika misahafu kwa mujibu wa imani zao pamoja na kile cha uadilifu chini ya Kamishna wa Sekretarieti ya maadili ya Viongozi wa umma.
Ni dhahiri kwamba kama wahenga wanenavyo lisemwalo lipo kama halipo laja, Rais amezungumza hayo kutokana na hali halisi ya wateule wengi wanavyofanya kazi zao kwa utashi binafsi badala ya kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa katika utendaji wao.
Baadhi ya watu wanapoteuliwa kushika nafasi fulani, hujisahau na kujifanya miungu watu, wakitaka wasujudiwe na wale wanaowaongoza huku wakitanguliza mbele maslahi binafsi ikiwamo kujilimbikizia mali, wakiendekeza ubadhirifu na matumizi mabaya ya madaraka. Wengine wamekuwa wakifanya vitendo vya ajabu vikiwamo ukandamizaji na unyanyasaji wa kijinsia kiasi cha kuwadhalilisha waliowateua na jamii kuona kama wametumwa kufanya hivyo.
Iko mifano ya baadhi ya wakuu wa mikoa na wilaya ambao wamekuwa wakitumia nafasi hizo vibaya kwa kuendekeza rushwa pamoja na kuwaweka ndani baadhi ya wananchi bila sababu zisizo na msingi. Kutokana na hulka hiyo, miongoni mwa wateule hao husema moyoni kwamba wameula kwa maana ya kujinufaisha kupitia vyeo hivyo badala ya kuwatumikia wananchi.
Mbali na vitendo hivyo, baadhi ya wateule wamekuwa wakilalamikiwa kutokujali matatizo ya watu wasio na uwezo badala yake wanawakumbatia wenye fedha pamoja na kushindwa kushughulikia kero za wananchi na matokeo yake kuendelea kuwa katika matatizo na kuzidi kuwa katika lindi la umaskini.
Kauli hiyo ya Rais Samia si mara ya kwanza kusikika katika jamii ya Watanzania. Aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa, pia aliwahi kusema katika miaka 10 ya uongozi wake, wateule wake wengi walishindwa kuheshimu na kuviishi viapo walivyokuwa wanakula wakati wakikabidhiwa majukumu ya uongozi.
Kwa hali hiyo, wateule wengi wamekuwa wakila viapo hivyo kwa mazoea ili kupata kile walichokuwa wakikitafuta lakini matendo yao yamekuwa tofauti na yale waliyoyatamka katika viapo vyao.
Ni wakati mwafaka sasa wateule hao wa Rais kubadilika kwa kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa viapo pamoja na kufuata maadili ya uogozi ambayo yameainishwa katika viapo vyao kama vile uaminifu, kutojihusisha na rushwa, kutotumia madaraka yao kwa huba na upendeleo.
Wateule hao wanapaswa kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia miiko iliyowekwa na kutambua kwamba uongozi ni utumishi na si kutumikiwa na pia wamepewa nafasi hizo kwa ajili ya kumsaidia Rais kutatua kero za wananchi ikiwamo kusimamia miradi ya maendeleo katika ngazi mbalimbali.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED