NI simulizi ngumu zilizojaa mateso kwa wanawake wenye tatizo la uvimbe kwenye kizazi (fibroids), wapo ambao wamefanyiwa upasuaji zaidi ya mara tatu lakini tatizo limerejea upya na wengine huishia kuwa wagumba.
Wanasimulia nyakati ngumu za maumivu makali wanazokutana nazo kila mwezi wakati wa hedhi, kupoteza damu nyingi na namna tatizo hilo linavyohatarisha ndoa zao na hali zao za kiuchumi.
Mkalimani wa lugha, Happy Dismas (33), mkazi wa Chang’ombe, Temeke mkoani Dar es Salaam ambaye hajajaliwa kupata mtoto hadi sasa, anasimulia namna anavyoshindwa kwenda ofisini wakati mwingine hadi siku nne kila mwezi kutokana na kutokwa damu nyingi wakati wa hedhi ikiambatana na maumivu makali.
Mwanamke huyu ambaye ni mwajiriwa katika ofisi binafsi, anasimulia kwamba, hali hiyo wakati mwingine inamletea shida kwa bosi wake.
Anasema kwa nafasi yake, asipohudhuria ofisini husababisha kuwapo mrundikano wa kazi na kusababisha baadhi ya huduma kusimama.
“Katika kitengo changu nipo mwenyewe kwa hiyo nisipokuwapo, kazi zinasimama. Wakati mwingine nikiwa ninapitia hali hii, ninalazimika kufanya kazi za ofisini nikiwa nyumbani, ili tu nisimkwaze bosi wangu,” anasimulia.
Happy anasema hali hiyo huchangia kuishiwa damu, kukosa raha na huwa kwenye msongo wa mawazo kwa sababu licha ya miaka minne nyuma kufanyiwa operesheni na kuondolewa uvimbe huo, umerejea tena.
“Daktari alinieleza ili kumaliza tatizo hili kabisa ninatakiwa kufanyiwa operesheni ya kuondolewa kizazi, jambo ambalo kwa kweli sikubaliani nalo kwa sababu ninahitaji kuzaa,” anasema.
Mfanyakazi wa benki, Luciana Kavishe (40), mkazi wa Mbezi, Dar es Salaam, anaweka wazi kwamba, tatizo hilo la uvimbe kwenye uzazi lilimsababishia kutoifurahia ndoa yake kwa miaka mitatu kutokana na kila alipopata ujauzito uliharibika.
Anasema kutokana na hali hiyo, mwaka jana baada ya kushika ujauzito wa tano alilazimika kwenda hospitalini kufanyiwa huduma ya kushonwa kizazi na kupewa huduma ya mapumziko (bedrest) hadi pale mimba ilipokomaa na kufanyiwa operesheni.
Luciana anasema tofauti na wengine ambao wanapojifungua kwa operesheni hutolewa na uvimbe, kwake ilishindikana na madaktari walimweleza sababu ni kwamba, uvimbe aliokuwa nao ulikuwa mkubwa, hivyo ungechangia kutokwa damu nyingi.
“Bado nina uvimbe mkubwa. Ninapitia changamoto kwa sababu ninalea mtoto mdogo huku nikipitia maumivu makali ya uvimbe. Ninalazimika kila siku kunywa dawa za kupunguza maumivu. Ninasubiri mtoto akue kidogo ili niende kuutoa,” anasimulia Luciana.
Simulizi hizo na madhila waliyopitia watangulizi haitofautiani na ya Maria Khamisi (45) mkazi wa Ilala, Dar es Salaam, aliyeishi na uvimbe wa namna hiyo kwa miaka 10, ingawa yeye anasema ilimchukua muda huo kutokana na kukosa fedha za matibabu.
Anasema alifanyiwa upasuaji na kutolewa uvimbe mwaka jana, baada ya ndugu zake kumchangia fedha kutokana na hali yake kuwa mbaya zaidi.
“Shida niliyopitia kwa miaka yote 10 ilipopatikana fedha ili nifanyiwe upasuaji niliwaambia madaktari watoe kizazi kwani sikutaka tena kupitia maumivu makali wala changamoto nilizopitia,” anasimulia.
Wakati simulizi hizo zikitolewa, ripoti ya Taasisi ya National Library Medicine (2024) inaonesha karibu asilimia 80 ya wanawake weusi kutoka nchi za Jangwa la Sahara wanapatwa na tatizo hilo na kusababisha changamoto kadhaa ikiwamo kukosa uwezo wa kubeba mimba.
KITAALAMU
Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Kinamama na Masuala ya Uzazi Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dk. Lilian Mnabwiru, anasema uvimbe unaojitokeza kwenye mfumo wa uzazi usipotibiwa mapema unaweza kuleta madhara makubwa kama vile kupungukiwa damu na ugumba.
Anasema uvimbe huo unaweza kutokea katika ngozi ya nje ya uzazi, misuli katikati au katika ngozi laini ya tumbo la uzazi la ndani anapokaa mtoto au katika mlango wa uzazi.
Anasema mara nyingi mwanamke anaweza kupata tatizo hilo anapokuwa katika umri wa uzazi wa miaka 18-40 kwa sababu ni kipindi ambacho mwili hutengeneza homoni za kike kwa wingi.
“Uvimbe huu husaidiwa kukua zaidi na homoni zijulikanazo kama Estrogen na Progesterone hasa katika umri wa uzazi. Mara nyingi hutokea katika familia yenye historia ya matatizo hayo na imegundulika kuwa wanawake wengi weusi wanapata sana hili tatizo” anafafanua mtaalamu huyo.
Anasema si rahisi kwa mwanamke mwenye tatizo hilo kujigundua mapema kwa sababu huwa hautoi dalili za moja kwa moja kama bado haujafikia saizi kubwa.
“Mwanamke anaweza kujiona amenenepa au anapata kitambi, kumbe uvimbe unakua taratibu kwa sababu unapokuwa upo katika saizi ndogo huwa hauleti madhara yoyote.
“Dalili ni maumivu ya tumbo la chini, kupata shida wakati wa kupata haja ndogo, kupata hedhi kwa muda mrefu na nyingi. Mtu anaweza kutumia hata pakiti mbili za pedi. Kutoshika mimba na huchangia upungufu mkubwa wa damu mwilini,” anasema.
Mtaalam huyo anasema mwanamke anaweza asipate ujauzito iwapo uvimbe utakuwa katika mlango wa kizazi ambapo huzuia mbegu za kiume zisiingie au endapo katika milango ya mirija kwa ndani itazuia utungaji wa mimba.
Kuhusu matibabu, Dk. Mnabwiru anasema yanategemea na umri wa mgonjwa na kama atakuwa anahitaji mtoto au laa au hutegemea ameathirika kwa kiwango gani.
“Mara nyingi uvimbe wenyewe ukiwa mdogo kuanzia sentimia moja au mbili huwa hauleti shida lakini kuanzia sentimita nne, tano, sita, saba inabidi kufanya matibabu kama itakuwa sentimita tatu ipo ndani ya mji wa mimba matibabu yake pia yapo.
“Kwa wale ambao hawana dalili kubwa, kuna matibabu mbadala. Kuna mfumo ambao tunautumia tunakwenda kutibu mishipa mikubwa inayosambaza damu kwenye kizazi na hivyo kufanya uvimbe usinyae,” anasema.
Matibabu mengine anayataja mtaalam huyo ni yanayohusisha mionzi maalum ya ‘ultrasound’ na pia, dawa za sindano au vidonge anahamasisha wanawake kujenga utamaduni wa kupima afya zao mara kwa mara kwa sababu dalili zake hazionekani mapema, huku akibainisha kwamba, asilimia kubwa ya wanaowagundua huwa hawajui kama wana uvimbe.
Anasema kwa siku wana kliniki ya wagonjwa 100 ambapo kati yao, hawakosekani wanawake 30 wenye tatizo hilo.
Daktari wa Afya katika Hospitali ya Aga Khan, Gregory Ntiyakunze, anasema zipo njia mbalimbali za kumtibu mgonjwa wa aina hiyo, lakini kwa yule anayetokwa na damu nyingi na hapendi kufanyiwa upasuaji, hupatiwa dawa za kuzuia hedhi kwa muda fulani, ili kumsaidia asipungukiwe damu anapokuwa katika hedhi.
Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Wanawake na Kizazi Hospitali Sant Francis Morogoro Dk. Elius Kweyamba, anasema asilimia 40 hadi 60 ya wanawake, wanaishi na uvimbe huo bila kujua na hawaoni athari yoyote.
Anasema katika kliniki yao mgonjwa umri mdogo waliyewahi kumwona ni mwenye umri wa miaka 25.
Dk. Kweyamba anasema operesheni kwa mgonjwa hutegemea na hali ya tatizo la mgonjwa na huweza kufanyiwa hata zaidi ya mara tatu.
“Wagonjwa ninaokutana nao katika kliniki yetu, kati ya 20 ninaowaona kwa siku, wenye tatizo huwa kati ya watu watatu hadi watano ikiwa ni asilimia 80 karibu ya kina mama wote wanaishi na tatizo hilo,” anasema.
MADHARA AFYA AKILI
Mwanasaikolojiatiba kutoka Kituo cha Afya cha Somedics Polyclinic, Saldeen Kimangale, anasema wanawake wengi wanaougua ugonjwa huo, wanapitia tatizo la afya ya akili, kwa sababu huwaathiri katika nyanja mbalimbali na kudumaza uwezo wao wa kukua kijamii.
Anasema hukabiliwa na mabadiliko makubwa na ya mara kwa mara na wakati mwingine ya ghafla yanayohusiana na kihisia, huzuni, hasira, tafrani, uchungu na maumivu.
Kimangale anasema husababisha kushindwa kutekeleza majukumu yao ya kila siku ikiwamo uzalishaji mali, jambo linalodhoofisha ubora wa maisha yake.
“Gharama kubwa za matibabu na hofu ya kutokuwa na suluhisho la haraka, huongeza msongo wa mawazo na hivyo kuzidisha changamoto katika afya yake ya akili na ustawi wake wa kisaikolojia,” anasema.
Anakiri kwamba hupokea wagonjwa wa aina hii wanaohitaji tiba ya kisaikolojia ambapo huwapatia huduma ya kuwaimarisha kimtazamo na kihisia.
Kadhalika huwapatia tiba ya kuwaongoza wawe na uwezo wa kukabiliana na jambo moja baada ya jingine, kuwasaidia kutenganisha ugonjwa na wao binafsi.
“Katika tiba hizi tunawaongoza kutambua kuwa ugonjwa usiwe ndio tafsiri ya utu wao. Tunawasaidia kuwa na mtindo mzuri wa maisha utakaowapunguzia adha ya ugonjwa kwa sababu baadhi ya tabia huchochea tatizo au kulikuza.
“Lakini pia inapobidi tunahusisha familia ili waweze kumpatia msaada sahihi na kwa wakati hasa nyakati ambazo hisia zake zinakuwa zinabadilika,” anasema.
Mtaalam huyo anasema huwafundisha mbinu mbalimbali za kujipatia utulivu na kukabiliana na msongo wa mawazo na huwapa matumaini ya kushinda changamoto zinazotokana na uvimbe kwenye kizazi.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED