Amcharanga mapanga mkewe kisha kunyonga kisa mapenzi

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 07:21 PM Mar 18 2024
Mtu akiwa ameshika panga.
PICHA :Mtandao
Mtu akiwa ameshika panga.

MWANAMKE mmoja aliyefahamika kwa jina la Doto Hamisi Magambazi (30) mkazi wa Mjimwema Kiluvya mkoani Pwani, amefariki dunia wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Tumbi baada ya kushambuliwa kwa kukatwa na panga sehemu mbalimbali za mwili wake.

Kulingana na taarifa iliyotolewa na Jeshi la Polisi mkoani humo, imeeleza kuwa baada ya uchunguzi wa awali uliofanywa na Jeshi hilo, ilibainika kuwa aliyehusika na shambulio hilo ni mume wake, aitwaye Mbaraka Haruna Mapunda (42), mkazi wa Chanika mkoani Dar es Salaam, aliyetalakiana nae mwaka mmoja uliopita, huku chanzo kikitajwa kuwa ni wivu wa mapenzi na kugombea mali walizochuma pamoja.

Wakati jeshi hilo likiendelea na msako wa kumakamata mtuhumiwa, ilibainika kuwa mtuhumiwa huyo alikuwa amejinyonga umbali wa mita 300 kutoka nyumbani kwa Doto Magambazi, Mtaa wa Mjimwema Kiluvya, kwenye kichaka kwa kutumia mkanda wa nguo kwa kujininginiza kwenye mti.