Yanga yapunguzwa kasi jeshini

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 10:40 AM Apr 25 2024
news
Picha: Mpigapicha Wetu
Kiungo mshambuliaji wa Yanga, Maxi Nzengeli, akimtoka nyota wa JKT Tanzania, Matheo Anthony (aliyelala chini), katika mechi ya Ligi Kuu Bara iliyochezwa kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Dar es Salaam jana.

VINARA wa Ligi Kuu Bara, Yanga wamepunguzwa kasi katika mbio za kuusaka ubingwa baada ya kulazimishwa suluhu na 'Maafande' wa JKT Tanzania katika mechi kali iliyochezwa kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo ulioko Mbweni, Dar es Salaam jana.

Mechi hiyo ilichezwa jana baada ya juzi kushindikana kutokana na sehemu kubwa ya uwanja huo kujaa maji yaliyotokana na mvua zinazoendelea kunyesha Dar es Salaam na Kamisaa wa mchezo, Kamwanga Tambwe, kuuahirisha.

Matokeo hayo yanaifanya Yanga kupoteza pointi mbili, sasa imefikisha pointi 59, ikiendelea kupepea juu ya msimamo wa ligi huku JKT Tanzania wamepanda nafasi mbili juu, ikitoka nafasi ya 15 na sasa ipo nafasi ya 13 baada ya kufikisha pointi 23.

Mabingwa hao watetezi, Yanga wanahitaji pointi 16 katika mechi zake saba zilizobakia ili kutawazwa mabingwa kwa mara ya tatu, kwa sababu watafikisha pointi 74 ambazo hazitafikiwa na timu yoyote ile.

Azam yenye pointi 54, ikishinda mechi zake sita ikafikisha jumla ya pointi 72, wakati Simba ikishinda mechi zake tisa itafikisha pointi 73.

Hata hivyo, mechi hiyo ilichezwa kwenye uwanja uliojaa matope na kufanya wachezaji kushindwa kuonyesha ufundi, vipaji na ubunifu na badala yake kucheza kwa jinsi unavyoruhusu.

Mara kwa mara wachezaji walishindwa kupiga chenga huku wengine wakianguka wenyewe au kushindwa kukaba kwa urahisi, wakati mwingine kupigwa chenga nyepesi, wakiteleza na kuanguka wenyewe wakati wa kukokota mpira.

Dakika 10 za mwanzo hakuna timu yoyote kufika langoni mwa mwenzake mpaka dakika ya 11, Yanga ilipofanya hivyo kwa shambulizi ambalo lilizaa kona ambayo haikuzaa goli.

Mpira wa kona uliopigwa uliokolewa na mabeki wa JKT Tanzania, lakini ukakwama katika matope mbele ya mshambuliaji, Stephane Aziz Ki, ambaye alipiga shuti kali kwa mguu wa kushoto ukawababatiza tena mabeki, kabla ya kuuokoa.

Dakika mbili baadaye, Augustine Okra, alikosa bao, baada ya kichwa alichopiga kuunganisha krosi ya Yao Kouassi kutoka nje kidogo ya lango.

JKT Tanzania ilifika langoni kwa Yanga mara ya kwanza katika dakika ya 15, baada ya George Wawa kuambaa na mpira katika wingi ya kulia, akapiga krosi iliyobabatiza mabeki wa vinara hao wa ligi, nusura mpira ujae wavuni kama si kipa, Djigui Diarra, kuwa makini na kuunyaka mpira huo.

Kuanzia dakika ya 30, JKT Tanzania ilionekana 'kuchangamka' kwa Yanga kufanya mashambulizi kadhaa ambayo yalionekana hatari ingawa hayakuzaa mabao.

Kama wachezaji wa timu hiyo wangekuwa makini wangepata bao dakika ya 34, kupitia kwa Said Ndemla ambaye alikimbia na mpira katika wingi ya kulia na kuingia ndani kidogo kabla ya kuachia shuti kali lililomparaza Diarra, lakini liliambaa pembeni na kutoka nje.

Dakika nne baadaye, maafande hao walifanya shambulio la hatari, ambapo kama si uimara wa beki, Ibrahim Hamad 'Bacca' aliyekuwa akijitosa kuzuia mashuti matatu yaliyokuwa yakipigwa na kumbabua kichwani na mwilini, wangeweza kuandika bao.

Kipindi cha pili Yanga waliingia kwa nguvu kufanya mashambulizi, huku JKT Tanzania nao wakibadilisha mfumo kwa 'kupaki basi'.

Ilikuwa ni dakika ya 57 ambapo Yanga ilikaribia kupata bao kupitia kwa, Maxi Nzengeli, aliyekuwa ndani ya eneo la hatari, akapiga shuti kali lililopanguliwa na kipa, Jacob Suleiman, lakini ulitua mbele ya lango na kusababisha kizaazaa cha piga nikupige, lakini alifanikiwa tena kuudhibiti mikononi.

Timu zote zilifanya mabadiliko ambayo yalionekana kutoathiri mwenendo wa mchezo, huku kila timu ikikosa mabao.

Sixtus Sabilo, ataikumbuka nafasi aliyopata dakika ya 75, alipopenyezewa pasi maridadi kutoka kwa Hassan Kapalata, akiwa anaangaliana na Diarra, alipaisha mpira juu, akiwa ndani ya eneo la boksi.

Aziz Ki aliunganisha vibaya mpira wa krosi kutoka kwa Kouassi dakika ya 79, ukaenda nje akiwa katika nafasi nzuri ya kuukwamisha mpira wavuni.

Yanga itajutia nafasi iliyokosa katika dakika tano zilizoongezwa, ambapo krosi iliyopigwa kutoka wingi ya kushoto ilimkuta, Joseph Guede, aliyeunganisha, lakini mpira ukaenda kugonga mwamba wa juu na kudunda chini katikati ya mstari na mwamba wa pembeni ukarejea uwanjani, kabla ya kipa Jacob, hajaudaka.