Yanga, Tabora Utd Mei Mosi

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 11:35 AM Apr 25 2024
Nembo ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
Picha: TFF
Nembo ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).

MABINGWA watetezi wa mashindano ya Kombe la FA, Yanga watacheza mechi ya hatua ya robo fainali ya michuano hiyo dhidi ya Tabora United ifikapo Mei Mosi kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.

Taarifa ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), jana limesema mechi tatu za hatua hiyo zitapigwa kwenye Uwanja wa Azam Complex, CCM Mkwakwani, Tanga na Liti, Singida.

"Mechi ya Yanga dhidi ya Tabora United itachezwa saa 2:30 usiku, ambapo kabla ya hapo zitakuwa zimepigwa mechi mbili, Ihefu ikikwaana na Mashujaa FC, Uwanja wa Liti, Singida, saa 10:00 jioni, kabla ya Coastal Union kuteremka Uwanja wa Mkwakwani, kukipiga dhidi ya Geita Gold, saa 12:15, jioni," taarifa ya TFF ilisema.

Wanafainali wa msimu uliopita, Azam FC wenyewe wanatarajia kushuka dimbani Mei 3, mwaka huu kwenye Uwanja wa Azam Complex kucheza dhidi ya Namungo FC.

Yanga ilitinga hatua ya robo fainali kwa kuifunga Dodoma Jiji mabao 2-0 wakati Tabora United waliibamiza Singida FG magoli 3-0, Azam yenyewe iliwachapa Mtibwa Sugar mabao 3-0, Ihefu ikawalaza KMC mabao 3-0 na Namungo iliwaondoa Kagera Sugar kwa penalti 5-3.

Mashujaa FC iliendeleza ubabe kwa Simba baada ya kuwaondoa kwa kuwafunga penalti 6-5, mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika, Kigoma.