Yanga kuongeza nguvu kiungo, beki wa kati

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 06:34 AM Aug 25 2024
Rais wa Klabu hiyo, Injinia Hersi Said.
Picha: Mtandao
Rais wa Klabu hiyo, Injinia Hersi Said.

IMEBAINIKA kuwa klabu ya Yanga ina mpango wa kusajili kiungo mkabaji kwa ajili ya kusaidiana na Khalid Aucho na beki wa kati kubadilishana na nahodha Bakari Mwamnyeto kwenye kipindi cha dirisha dogo la usajili.

Taarifa hizo zimekuja baada ya majuzi, Rais wa Klabu hiyo, Injinia Hersi Said kuweka wazi kuwa wanampango wa kusajili wachezaji wawili wa kimataifa mwezi Desemba na Januari ambako kutakuwa na kipindi cha usajili wa dirisha dogo.

Rais huyo hakutaja maeneo ambayo anatarajia kusajili, lakini habari kutoka ndani ya klabu hiyo zinasema kuwa wanaotarajiwa kusajiliwa ni kiungo mkabaji na beki wa kati ambao watakuja kuongeza nguvu ndani ya kikosi.

Mtoa taarifa alisema kuwa atasajiliwa namba sita mwenye uzoefu wa mechi za kimataifa ili kusaidiana na Aucho, ambaye ndiye amekuwa mhimili kwa sasa na akikosekana pengo lake linaonekana.

"Akiumia au akiwa na kadi inakuwa shida sana, nakumbuka kuna michezo alikosa msimu uliopita kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika tulipata tabu, na hata ule msimu ambao tulicheza Kombe la Shirikisho Afrika mechi mbili za fainali dhidi ya USM Alger alikosekana kutokana na kadi na tuliukosa ubingwa, kwa maana hiyo tunakwenda kusajili mchezaji ambaye ana uwezo kama Aucho, au zaidi yake ili akikosekana yoyote kusiwe na pengo, Andambwile ni mzuri, lakini bado hana uzoefu sana kwenye michezo wa kimataifa," kilisema chanzo hicho.

Chanzo kimesema kuwa Yanga inahitaji pia beki wa kati wa kimataifa wa kusaidiana na Mwamnyeto, ambaye pia atamfanya Dickson Job kurejea kwenye namba za pembeni.

Yule beki 'Bacca' (Ibrahim Hamad), hana mpinzani, sasa pale tunataka Mwamnyeto na beki mwingine wawe wanabadilishana, tulimleta Gift Fred, lakini hakukidhi matarajio," alisema mtoa taarifa.

Hivi majuzi, Injinia Hersi alibainisha kuwa watashusha wachezaji wengine wawili kutoka nje ya nchi kwa ajili ya kukiongezea nguvu kikosi hicho, ingawa hakutaja maeneo watakayosajili.

"Kikosi hiki hakijakamilika, bado, nataka niwaambie tu, Yanga hii bado, tena kuna mchezaji tulitakiwa tumlete kwenye hili dirisha kubwa lakini dili halikukamilika, baada ya hapa, Januari kutakuwa na ongezeko la wachezaji wengine wawili wa kigeni. Kwa hiyo haijakamilika, ikikamilika ndiyo wanahabari tuulizeni kuhusu ubingwa wa Afrika, lakini kwa sasa bado, lengo letu ni robo fainali, tunataka tuingie makundi tuzoee kwanza makundi, halafu twende robo fainali, ila wakati mwingine Mungu huwa ana zawadi, akitupa nusu fainali, fainali au tukichukua ubingwa, sawa tutanashukuru," alisema." alisema Hersi.