Yanga, Azam fainali ya aina yake

By Shufaa Lyimo , Nipashe
Published at 07:18 AM Aug 11 2024
 Kocha wa Azam, Bruno Ferry na Kocha wa Yanga Migel Gamond.
Picha: Mtandao
Kocha wa Azam, Bruno Ferry na Kocha wa Yanga Migel Gamond.

WAKATI kocha wa Azam, Bruno Ferry akisema kikosi chake kipo tayari kuwakabili Yanga leo, kocha wa wapinzani wao hao, Miguel Gamondi, amesema anafurahia kukutana na mechi ngumu kwa kuwa inakifanya kikosi chake kuimarika zaidi.

Yanga na Azam zitakutana leo kwenye fainali ya Ngao ya Jamii kwenye mchezo utakaochezwa saa 1:00 usiku ukitanguliwa na mchezo wa kusaka nafasi ya tatu kati ya Simba na Coastal Union.

Yanga imetinga hatua hiyo baada ya kuifunga Simba bao 1-0 kwenye mchezo wa nusu fainali Alhamisi iliyopita huku Azam FC siku hiyo hiyo ikiiadhibu Coastal Union mabao 5-2 na kutinga fainali.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Gamondi, alisema mchezo dhidi ya Simba na huu wa leo unakisaidia kikosi chake kuimarika kutokana na ugumu na ubora wa wapinzani wao.

Alisema anatarajia kukutana na mchezo mgumu mbele ya Azam kwa wapinzani wao hao ni timu nzuri na anaiheshimu.

"Kwa upande wangu ninafurahi kukutana na timu yenye ushindani kama Azam FC kwa kuwa inakifanya kikosi changu kizidi kuwa bora zaidi, ninaomba mashabiki wetu waje kwa wingi uwanjani kuangalia burudani tutakayowapa," alisema Gamondi. 

Alisema makosa madogo madogo aliyoyabaini katika mchezo wao  wa nusu fainali dhidi ya Simba ameyafanyia kazi ili yasiweze kujirudia kwenye mchezo leo. 

Kwa upande wake Dickson Job ambaye alizungumza kwa niaba ya wachezaji wenzake alisema mchezo huo utakuwa na upinzani kutokana na timu zote kuwa na mabenchi bora ya ufundi. 

" Sisi wachezaji tunafahamu mchezo huo utakuwa mgumu hivyo tunaahidi kupambana ili tuweze kupata matokeo mazuri, alisema Job. 

Kwa upande wake, Kocha wa Azam, Ferry alisema wanatarajia kupata ugumu mbele ya wapinzani wao kwa kuwa ni timu inayofanya vizuri kwa sasa.

"Mchezo utakuwa mgumu sitaki kuzungumzia Yanga kwa kuwa hakuna mtu asiyefahamu ubora wake, kikubwa ni kupata ushindi," alisema Ferry. 

Alisema wamejiandaa na wapo tayari kukutana na yanga kwenye mchezo huo wa leo.