Kibu aitamani Yanga mapema

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 09:32 AM Sep 30 2024
Winga wa Simba, Kibu Denis.
Picha:Mtandao
Winga wa Simba, Kibu Denis.

WAKATI mechi ya watani wa jadi ikitarajia kuchezwa Oktoba 19, mwaka huu, winga wa Simba, Kibu Denis, amesema anatamani siku ifike upesi kwani anapenda sana kucheza mechi za dabi.

Kibu, ambaye hivi karibuni aliingia kwenye mzozo na klabu yake kwa kutoroka kwenda nje ya nchi kwa ajili ya kujaribu kucheza soka la kulipwa kabla ya kurejea, alisema moja ya mechi ambazo anapenda sana kucheza ni dhidi ya Yanga.

Amebainisha kuwa mara nyingi 'dabi' ikifika yeye anakuwa kwenye wakati mzuri sana, na anakuwa na hamu ya kutaka kuwaonesha mashabiki nini anakitoa kwa timu yake.

"Mimi katika mechi ambayo huwa napenda zaidi kucheza ni dhidi ya Yanga, yaani mchezo wa 'dabi' wa timu hizi mimi ndiyo nazipenda sana kuliko zingine, kwa hiyo naisubiri kwa hamu," alisema mchezaji huyo ambaye alisajiliwa akitokea Mbeya City mwaka 2021.

Alibainisha hata kuumia mara kwa mara katika michezo baina ya timu hizo, inatokana na jinsi anavyojitolea, lakini hana ugomvi na mtu kwani yanayotokea yote ni mambo ya soka.

"Ni mechi ambazo huwa zikifika na mimi natakiwa kucheza huwa niko kwenye 'mudi' sana, nakuwa nimejiandaa vizuri nataka niwaoneshe mashabiki uwezo wangu na huwa najitoa, napambana hadi tone la mwisho la damu.

"Nafikiri hata ninavyoumia ni kwa sababu hiyo, nakumbuka nilivyogongana na Kibwana Shomari mechi moja, na ile ambayo niliumizwa na kipa wa Yanga, Djigui Diarra.

Kibu aligongana na Kibwana katika mchezo wa raundi ya pili ya Ligi Kuu Tanzania Bara uliochezwa Aprili 16, 2023, msimu wa 2022/23, Simba ikishinda mabao 2-0 na wote wawili walipata majeraha.

Mchezaji huyo pia aliumizwa na kipa Diara katika mechi ya raundi ya kwanza msimu uliopita uliochezwa, Novemba 6, mwaka jana, Yanga ikishinda mabao 5-1.

Mechi zote hizo, Kibu alifunga mabao, akipachika bao la pili katika mechi ambayo Simba ilishinda 2-0 na bao la kufutia machozi ilipofunga 5-1, lakini hakuweza kumaliza baada ya kufanyiwa madhambi.

"Kwa hiyo naisubiri kwa hamu ili niwathibitishie mashabiki wa Simba kuwa mimi niko na wao," alisema.

Kibu pia aliuzugumzia mchezo wao dhidi ya Al Ahli Tripoli uliochezwa hivi karibuni kuwa ulikuwa mgumu mno tofauti na wengi walivyofikiria.

"Hata lile bao ukiangalia lililifunga kwenye mazingira magumu, lilikuwa gumu, halikuwa rahisi kufunga, lakini haikuwa rahisi kuuzuia ule mpira, nilishukuru sana kufunga lile bao, ila niseme hakukuwa na muda wa kushangilia kwa sababu lilikuwa la kusawazisha ingawa lilituamsha zaidi wachezaji, halikutakiwa kuwa na mbwembwe za kushangilia.

"Al Ahli Tripoli ilikuwa na wachezaji wakubwa ambao wana uzoefu sana, tulichokuwa wachezaji tunakipambania ni kuvuka kwenye hatua ya mtoano na kuingia makundi, umoja wetu umetusaidia," alisema winga huyo mwenye nguvu ya kupiga mashuti kwa miguu yote.