Stars na sababu za kuiua Ethiopia leo kufuzu Afcon

By Faustine Feliciane ,, Shufaa Lyimo , Nipashe
Published at 07:51 AM Sep 04 2024
Kaimu Kocha Mkuu, Hemed Morocco.
Picha: Mtandao
Kaimu Kocha Mkuu, Hemed Morocco.

KIKOSI cha Timu ya Taifa ya Tanzania 'Taifa Stars', leo kinaanza kampeni ya kusaka tiketi ya kushiriki Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025, kitakapocheza dhidi ya Ethiopia huku Kaimu Kocha Mkuu, Hemed Morocco, licha ya kuweka wazi kuwa wamejiandaa na wapo tayari kwa mchezo huo, lakini pia akitoa sababu kwa nini ni muhimu kwao si tu kushinda bali kufuzu fainali hizo.

Stars itawakaribisha Wahabeshi hao kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa kuanzia majira ya saa moja usiku huku ikiwa na lengo moja kuu la kuanza na ushindi nyumbani katika harakati hizo za kuwania kufuzu AFCON 2025.

"Tumejiandaa vizuri, ni mchezo muhimu sana kupata matokeo nyumbani, kushinda mchezo wa kwanza kutazidi kutuongezea kujiamini, nashukuru Mungu wachezaji wote wapo vizuri na kila mmoja anautaka mchezo huu," alisema Morocco.

Aidha, alisema wanakutana na Ethiopia leo huku wakiwa hajwakutana kwa muda mrefu na hiyo itaongeza ugumu wa mchezo huo, lakini wapo tayari kupambana.

"Wapinzani wetu tupo nao Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, lakini ukweli hatujakutana nao muda mrefu, tunajua wana kikosi kizuri na wameimarika zaidi, wanacheza kitimu, lakini sisi tunaanza, tumejianda na kujipanga vizuri, tunataka kuanza vizuri safari yetu kuelekea kwenye fainali hizo huko Morocco," alisema Morocco.

Aliweka wazi kuwa wamefanikiwa kuwafuatilia katika michezo michache ya hivi karibuni kupitia mikanda ya video na hiyo imewasaidia kujipanga vizuri kuvuna pointi tatu.

"Ni muhimu sana sisi kama Tanzania kufuzu fainali za mwakani, tunajiandaa kuandaa fainali za mwaka 2027, itakuwa na maana kubwa sana tukifuzu fainali za Morocco," alisema kocha huyo.

Kwa upande wa mwakilishi wa wachezaji, Dickson Job, alisema wapo tayari kwa ajili ya mchezo huo na kudai watapambana kwa asilimia 100 kuweze kupata pointi tatu.

"Kwa upande wetu sisi wachezaji, tumejipanga vizuri kuhakikisha tunafanya vizuri katika mchezo huu, lengo ni kuanza vizuri mchezo wetu wa kwanza," alisema Job.

Katika mechi tatu za mwisho za hivi karibuni, Stars haijapata ushindi mbele ya Ethiopia ikitoka sare michezo miwili na kufungwa mmoja.