Simba yawafuata simba Mikumi kuzindua wiki yao

By Shufaa Lyimo ,, Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 07:54 AM Jul 23 2024
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Klabu ya Simba, Iman Kajula.
Picha: Simba SC
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Klabu ya Simba, Iman Kajula.

HUKU ikimrejesha meneja wake wa zamani, Patrick Rweyemamu, katika nafasi hiyo, Klabu ya Simba kesho inatarajia kuzindua wiki ya tamasha lao la kila mwaka lijulikanalo kama, Simba Day, kwenye Hifadhi ya Mbuga za Wanyama, Mikumi mkoani Morogoro.

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Klabu ya Simba, Iman Kajula, alisema wameamua kwenda kuzindua wiki yao mkoani Morogoro kutokana na kutambua kuwa wao kama Watanzania wana jukumu la kutangaza vivutio vya utalii hapa nchini.

"Sisi kama Simba tunafahamu jukumu la kutangaza utalii kwani Tanzania ni nchi ya tatu kwa kuwa na vivutio vingi vya utalii, vile vile tunaunga mkono serikali kutangaza utalii wetu," alisema Kajula.

Naye Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi ya Mikumi, Agustino Masesa, aliishukuru Simba kwa heshima waliyowapa kwenda kuzindua wiki yao katika hifadhi hiyo ambayo Agosti 7, mwaka huu, inafikisha miaka 60.

Akielezea utaratibu mzima wa uzinduzi huo, Meneja Habari na Mawasiliano wa klabu hiyo, Ahmed Ally, alibainisha kuwa wanachama na mashabiki wa Simba watasafiri kwenda Morogoro na treni ya umeme (SGR), alfajiri siku ya uzinduzi (leo).

"Tumetenga mabehewa matatu maalum kwa ajili ya mashabiki wetu na kila shabiki atasafiri bure hakutakuwa na malipo yoyote kwa ajili ya safari hiyo," alisema.

Hata hivyo, alisema kuingia kwenye hifadhi kila shabiki atalipia kiasi cha shilingi 5,900 kwa ajili ya kuingia ndani ya Hifadhi ya Utalii Mikumi kuangalia wanyama.

Aidha, alitangaza viingilio vya kuingia uwanjani kuangalia mchezo wao, Simba Day dhidi ya APR (Rwanda) kuwa mzunguko ni Sh. 5,000, machungwa Sh. 10,000, VIPC Sh. 20,000, VIP B Sh. 30,000 VIP A Sh. 40,000, pamoja Platinum ambayo ni Sh. 200,000, huku akiweka wazi kuwa tiketi zimeanza kuuzwa tangu jana. 

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli nchini (TRC), Masanja Kadogosa, aliishukuru Klabu ya Simba kwa kuamua kusafirisha wanachama na mashabiki wake kwa usafiri huo kwani itawapa faida kubwa sana kibiashara kwa kuwa tukio litaangalia na mamilioni ya watu nchini na nje ya nchi.

"Tutashirikiana na watu wote wanaotaka kwenda na kurudi Morogoro na hata ukiangalia nauli zetu ni rafiki Sh. 13,000 tu. Tunawashukuru sana kwa tukio hili, ni tukio la kizalendo, kwa sisi SGR ni jambo kubwa tunahitaji kuonekana," alisema Mkurugenzi huyo.

Uzinduzi huo ni kuelekea kwenye kilele cha tamasha la 16 la Simba Day, ambapo huanza kwa wiki nzima wanachama na mashabiki katika matawi yote nchini kufanya kazi za kujitolea kwa jamii na kutoa misaada mbalimbali kwa wahitaji, kabla ya siku husika ambapo mwaka huu itakuwa ni Agosti 3.

Siku ya kilele mashabiki na wanachama hukusanyika Uwanja wa Benjamin Mkapa tangu asubuhi ambako huwa na burudani mbalimbali, wasanii, muziki, ngoma, na michezo mbalimbali, ikiwamo kutambulishwa kwa kikosi kipya cha timu hiyo, kabla ya kuhitimisha kuingia uwanjani kucheza mechi, na mwaka huu itakipiga dhidi ya APR ya Rwanda.

Tamasha hilo lilianzishwa 2009, chini ya uongozi wa Hassan Dalali, na limebaki kuwa moja ya matukio makubwa ya kila mwaka nchini ambayo yamejipatia umaarufu kiasi cha klabu nyingi kwa sasa Afrika Mashariki na Kati kuiga.

Wakati huo huo, Klabu ya Simba imemrejesha kikosini Rweyemamu kuendelea na majukumu yake ya kuwa meneja wa timu hiyo.

Habari zilizopatikana jana jijini Dar es Salaam ndani ya klabu hiyo zinasema, Rweyemamu ambaye aliondolewa mwaka jana na kuwa Mkuu wa Programu za Soka la Vijana, alitarajiwa kuondoka jana kuelekea Misri kujiunga na kambi ya timu hiyo iliyoanza Julai 8, mwaka huu, kwenye mji wa Ismailia.

Anachukua nafasi ya Mikael Igendia raia wa Kenya ambaye alikuwa Meneja wa Simba na Mkuu wa Sayansi ya Michezo ambaye aliichukua nafasi yake kabla ya kurejeshwa.