MSAFARA wa watu 50, wakiwamo wachezaji 22 wa timu ya Simba, ulitarajiwa kupaa saa 10:00 alfajiri ya leo kuelekea nchini Tunisia kwa ajili ya mchezo wao wa raundi ya nne, Kombe la Shirikisho Afrika hatua ya makundi dhidi ya CS Sfaxien, huku Meneja Habari wa Klabu hiyo, Ahmed Ally, akisema hawahitaji matokeo mengine zaidi ya ushindi kwenye mchezo huo.
Simba ambayo itapitia nchini Uturuki kabla ya kwenda Tunisia, inatarajiwa kucheza mechi hiyo Jumapili ijayo Januari 5 kwenye Uwanja wa Olympique Hammadi Agrebi kwenye mji Rades saa 1:00 usiku kwa saa za Tanzania.
Ahmed, alisema matokeo ya mchezo huo ndiyo yatatoa dira na taswira ya kuelekeza kwenye hatua ya robo fainali au la.
Alisema ugumu wa mchezo huo utatokana na kwamba CS Sfaxien wanataka kuutumia mchezo huo ili kurudi kwenye njia baada ya kupoteza michezo yake yote mitatu iliyopita.
"Kundi ni gumu kwa sababu timu zote nne zina uhakika wa kwenda robo fainali, timu tatu zinafanana kwa pointi, mechi yetu dhidi ya CS Sfaxien ndiyo itaanza kuonyesha utofauti nani awe kwa kwanza na nani wa pili kwenye kundi yupi wa tatu na yupi abaki mkiani.
Kwetu Simba huu mchezo ndiyo unakwenda kutengeneza dira au taswira ya kuelekea hatua ya robo fainali, ni mechi ngumu kwa sababu mpinzani wetu anataka kuifanya mechi hii kwake iwe na kuamkia. Ni muhimu kwetu kwenda na nguvu zote kuhakikisha tunapata ushindi katika mchezo huu, tukishinda tutakuwa tumemuondoa kabisa CS Sfaxien katika mbio za kuwania robo fainali na kujiweka kwenye nafasi nzuri ya kufuzu kutoka kwenye Kundi A," alisema Ahmed.
Alisema kuwa, si kwa Sfaxien tu, pia wamejidhhatiti kutopoteza mechi nyingine dhidi ya Bravo do Maquis ya Angola na CS Constantine ya Algeria.
Simba iko Kundi A, ikiwa nafasi ya tatu katika msimamo, ikikusanya pointi sita sawa na kinara wa kundi, Bravo do Maquis na CS Constantine ambayo ipo nafasi ya pili lakini zikitofautiana mabao ya kufunga.
Bravo do Maquis ina mabao sita, CS Constantine ikifunga matano, huku Simba ikifunga manne, CS Sfaxien ikiwa haina pointi.
Wakati huo huo, Ahmed, alisema tayari winga, Elie Mpanzu amekamilisha usajili kwenye michuano ya kimataifa, hivyo atakuwepo kwenye mchezo huo.
Mpanzu ambaye tayari ameshaanza kukipiga kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara baada ya taratibu zake kukamilika, amekamilisha pia usajili kwa ajili ya Kombe la Shirikisho.
"Nawatoa wasiwasi wanachama na mashabiki wa Simba kuhusu Mpanzu, taratibu zote za kucheza michuano ya kimataifa nayo pia imekamilika kwa hiyo atakuwa mmoja wa wachezaji watakaoenda kutuwakilisha nchini Tunisia," alisema.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED