BAADA ya kutinga hatua ya robo fainali ya mashindano ya Kombe ya FA, Kocha Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi, amesema kwa sasa anajipanga kuhakikisha anaondoka na pointi tatu muhimu katika mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Singida Fountain Gate FC itakayochezwa keshokutwa.
Kwa upande wa Simba iliyoondolewa katika michuano ya Kombe la FA na Mashujaa FC ya Kigoma hapo juzi, pia imetangaza 'vita' kwa kusema inaelekeza akili na mipango yake yote kuhakikisha inafanya vizuri katika mechi zote za Ligi Kuu Tanzania Bara zilizobakia.
Yanga imesonga mbele katika michuano ya Kombe la FA baada ya kuifunga Dodoma Jiji FC mabao 2-0, mechi ikichezwa kwenye Uwanja wa Jamhuri jijini, Dodoma huku Simba ikitupwa nje ya mashindano hayo kwa kufungwa penalti 6-5 na Mashujaa.
Akizungumza na gazeti hili jana, Gamondi, alisema ugumu waliokutana nao katika michezo ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Mamelodi Sundowns umewasaidia kupata matokeo chanya walipokutana na Dodoma Jiji FC.
Gamondi alisema sasa anageuzia nguvu zake kuhakikisha wanavuna pointi tatu katika mchezo huo wa Ligi Kuu ili kuendelea kujiimarisha kwenye vita ya kutetea ubingwa wa ligi hiyo wanaoushikilia.
"Nimefurahi kupata matokeo chanya katika mchezo mgumu dhidi ya Dodoma Jiji FC na kusonga mbele, haikuwa mechi rahisi kutokana na ugumu wa wapinzani wetu walivyokuwa," alisema Gamondi.
Aliongeza Yanga ilikuwa na kipindi kigumu kwa dakika zote 90 kutokana na Dodoma Jiji kuwa imara na hali hiyo ilitokana na kikosi chao kuundwa na idadi kubwa ya wachezaji vijana lakini walifanikiwa kucheza kwenye mipango yao na kupata ushindi.
“Ni mechi nzuri, niwapongeze wachezaji wangu, lakini bado tuna kazi nyingi mbele, kuna mechi ya ligi tunaenda kucheza, muda ni mfupi wa maandalizi, tunatakiwa kuwa makini kwa kila mechi ili kupata matokeo mazuri hasa katika ligi kwa lengo la kutetea taji letu,” alisema kocha huyo raia wa Argentina.
Kuhusu kurejea, Khalid Aucho, alisema ameanza kumpa nafasi ya kucheza dakika chache kiungo huyo baada ya kupona majeraha, amefanya vizuri katika mchezo wa juzi.
Ofisa Habari wa Yanga, Ali Kamwe, alisema hali ya Pacome Zouzoua ni nzuri na anatarajiwa kuwa sehemu ya kikosi cha mchezo dhidi ya watani wa jadi Simba utakaochezwa Aprili 20, mwaka huu.
Kamwe alisema Aucho amepona na tayari aneanza kucheza na hivi karibuni wanatarajia kumuona urejeo wa Pacome wakitarajia kumuona uwanjani Aprili 20 mechi dhidi ya Simba.
"Pacome yupo na Aprili 20, mwaka huu katika mchezo wetu dhidi ya Simba atakuwa sehemu ya kikosi baada ya kupona na kuanza mazoezi ya ushindani na kugongana," alisema Kamwe.
Naye Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, alisema baada ya kutupwa nje katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la FA, sasa viongozi, benchi la ufundi na wachezaji 'wanakusanya' nguvu kwa ajili ya kupambana ili kupata ubingwa wa Bara.
Hata hivyo Simba tayari inashikilia taji moja msimu huu ambalo ni la Ngao ya Jamii baada ya kuwafunga Yanga penalti 3-1, katika mechi ya fainali ya michuano hiyo iliyochezwa Agosti 13, mwaka huu kwenye Uwanja wa CCM Mkwakwani, Tanga.
"Hivi sasa Simba imebakiwa na chaguo moja au taji moja la kulipigania nalo ni la Ligi Kuu Tanzania Bara, tumepoteza mataji mengine yote ambayo yalikuwa katika mikono yetu na tulikuwa tunayapigania, taji pekee lililo mikononi mwetu ni hili.
Yapo maneno mengi, wapo wanaosema wamekata tamaa, lakini niseme bado tunayo nafasi kubwa katika ligi ili tukianguka tuwe wote pamoja na kama tukifaulu, tufaulu pamoja tufurahi wote," alisema Ahmed.
Simba inajiandaa kucheza dhidi ya Singida Black Stars (zamani Ihefu), katika mechi ya Ligi Kuu Bara itakayochezwa kesho kwenye Uwanja wa CCM Liti mkoani, Singida.
Aliongeza hali ya Henock Inonga imeimarika na atarejea katika kikosi huku akimtaja kipa, Aishi Manula, ndiye anabakia mchezaji atakayekuwa kuwa nje ya uwanja kwa muda mrefu.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED