Simba Queens, Yanga Princess dabi ya kisasi

By Saada Akida , Nipashe
Published at 11:20 AM Apr 25 2024
Kocha Msaidizi wa Simba Queens, Mussa Hassan ‘Mgosi',.
Picha: Maktaba
Kocha Msaidizi wa Simba Queens, Mussa Hassan ‘Mgosi',.

“WANAENDA kulipa kisasi cha kaka zetu". Hiyo ni kauli ya Kocha Msaidizi wa Simba Queens, Mussa Hassan ‘Mgosi', kuelekea mechi ya Ligi Kuu ya Soka ya Wanawake Tanzania dhidi ya watani zao wa jadi, Yanga Princess itakayochezwa leo kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.

Vinara Simba Queens wenye pointi 31 watashuka uwanjani leo wakiwa na kumbukumbu ya ushindi wa mabao 3-1 walioupata katika mechi ya kwanza wakati Yanga Princess wako nafasi ya tatu katika msimamo wa ligi hiyo wakiwa na alama 21.

Licha ya mchezo huo kuwa dabi, Simba Queens wamejipanga kuhakikisha wanalipa kisasi cha 'kaka zao' Simba ambao walikubali kipigo cha pili msimu huu dhidi ya Yanga.

Akizungumza jijini jana, Mgosi alisema wamejiandaa vizuri kusaka pointi tatu muhimu lakini kubwa kwao no kulipa kisasi walichofanyiwa kaka zao, Simba.

Mgosi alisema wamefanya maboresho ba kusahihisha mapungufu waliyoyabaini katika kikosi chao na wataingia tofauti na namna walivyocheza mechi yao ya mwisho dhidi ya Baobab Queens.

“Yanga Princess wapo vizuri lakini hata  Simba Queens tuko vizuri kupambania malengo yetu, tunahitaji kutwaa ubingwa, hatuwezi kufikia hapo hadi kuvuna pointi tatu katika kila mechi, mashabiki wanatakiwa kujitokeza kwa wingi kutuunga mkono.

Kufuatia  kile ambacho wamekipata kwa kaka zetu wikiendi iliyopita na mashabiki wetu kupata maumivu tunawahakikisha tunaenda kulipa kisasi cha kaka zetu, hatuna kazi mbovu, tunaenda kucheza soka safi lakini kuhakikisha tunawapa furaha mashabiki wetu,” alisema Mgosi

Nahodha wa Simba Queens, Violeth Nicholaus, alisema wamejipanga vizuri sio kwa mchezo wa leo pekee, ila wanahitaji kutafuta pointi tatu mbele ya mpinzani yoyote wanayekutana naye katika ligi hii.

“Msimu huu tunahitaji kufanya vizuri kila mechi, makocha wamemaliza kazi yao, jukumu letu wachezaji ni kuhakikisha tunafanikiwa kusaka alama tatu katika kila mchezo ukiwamo dhidi ya Yanga Princess, hautakuwa mchezo rahisi, tutacheza kwa tahadhari kufikia malengo yetu,” alisema Violeth. 

Kocha Msaidizi wa Yanga Princess, Fred Mbuna, alisema vijana wako salama na wamejiandaa vizuri na mechi hiyo ambayo wataingia 'kikubwa' kuhakikisha wanafuta 'unyonge' mbele ya wapinzani wao.

Mbuna alisema wanaangalia zaidi kusaka  matokeo ya leo licha ya Simba Queens kuwa imara katika safu ya ushambuliaji wao wamejipanga vyema kuhakikisha hawaruhusu kufungwa.

“Tunatambua hii ni dabi, ni mchezo mkubwa sana, katika michezo kadhaa tumekuwa hatupati matokeo lakini tumejipanga safari hii tunaenda kufanya kile kilichofanywa na timu ya wanaume,” alisema Mbuna.

Bingwa wa ligi hiyo atapata tiketi ya kuiwakilisha Tanzania Bara katika Ligi ya Mabingwa wa Afrika Mashariki na Kati (CECAFA).