MASHINDANO ya kuwania Ngao ya Jamii kwa Wanawake yamepangwa kufanyika kuanzia Septemba 24 hadi 27, mwaka huu kwenye Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam.
Ofisa Habari na Mawasiliano wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Clifford Ndimbo, alisema jana mashindano hayo yanayofanyika kwa mara ya pili yatashirikisha timu nne zilizomaliza katika nafasi ya juu kwenye msimu uliopita.
Ndimbo alizitaja timu zitakazoshiriki mashindano hayo ni pamoja na mabingwa wa Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania (TWPL), Simba Queens, JKT Queens, Yanga Princess zote kutoka Dar es Salaam na Ceasiaa ya mkoani Iringa.
"Tunatarajia kufungua pazia la msimu mpya wa Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania kwa mashindano ya Ngao ya Jamii, maandalizi yake yanaenda vizuri na michuano hii itaanza kwa kushirikisha klabu nne, tunaamini yatakuwa na ushindani na msisimko mkubwa zaidi ya mwaka jana," Ndimbo alisema.
Naye Meneja wa Simba Queens, Selemani Makanya, alisema timu yake iko tayari kwa ajili ya kutetea taji hilo waliloshinda mwaka jana.
Makanya alisema wanaamini watafanya vyema katika mashindano hayo kwa sababu wachezaji wao bado wana 'joto' la michuano ya Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), iliyomalizika wiki iliyopita.
"Hakuna mashindano rahisi, tunajua kila timu imejiandaa kufanya vyema, tutakiwa kama washindani, hatutabweteka, tunahitaji kuanza msimu mpya kwa kubeba ngao hiyo," Makanya alisema.
Simba Queens itamkosa kipa wake chaguo la kwanza Mkenya, Caroline Rufa, ambaye aliumia katika michuano ya CECAFA iliyomalizika huko Ethiopia kwa wenyeji CBE kutwaa ubingwa.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED