Simba kurudia ya 1993 Angola?

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 08:54 AM Jan 11 2025
 Simba kurudia ya 1993 Angola?
Picha:Simba
Simba kurudia ya 1993 Angola?

KIKOSI cha Simba kesho saa 1:00 usiku kinatarajia kushuka kwenye Uwanja wa Novemba 11, Luanda, Angola kufanya kile ilichokifanya miaka 31 iliyopita ilipofanikiwa kufuzu hatua ya fainali ya Kombe la CAF, ambalo sasa linaitwa Kombe la Shirikisho, dhidi ya Atletico Spotivo Aviacao, ikiwa ugenini.

Simba itacheza mechi ya raundi ya tano, Kombe la Shirikisho barani Afrika hatua ya makundi dhidi ya Bravos do Maquis ya nchini humo katika mchezo ambao inahitaji ushindi au sare ili kufuzu hatua ya robo fainali kutoka Kundi A.

Kama itafanikiwa kufanya hivyo, itakuwa ni mara ya pili kwani mwaka 1993, Simba ilifanikiwa kuingia hatua ya fainali ya Kombe la CAF, ilipotoka suluhu dhidi ya Atletico Spotivo Aviacao ikiwa nchini humo, katika mchezo wa marudiano baada ya mchezo wa kwanza uliochezwa Uwanja wa Taifa Dar es Salaam (sasa Uhuru), Simba kupata ushindi wa mabao 3-1.

Iwapo itapata ushindi pia itakuwa ni mara ya pili kwani ikiwa nchini humo, Oktoba 9 mwaka 2022, iliichapa Primeiro de Agosto mabao 3-1, katika mchezo wa raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa huku wa marudiano uliochezwa nchini, Oktoba 16, 2022, Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, ilishinda bao 1-0, na kufanikiwa kutinga hatua ya makundi.

Kocha Mkuu wa Simba, Fadlu Davids, amesema maandalizi yote ya mchezo huo yamekamilika huku akisema atakwenda kuikabili Bravos do Maquis kwa mfumo tofauti.

Alisema kuwa timu hiyo ni hatari inapokuwa nyumbani, ikipenda zaidi kumiliki mpira, hivyo ametengeneza mkakati wa kuhakikisha wanawanyima fursa hiyo.

"Mechi itakuwa ngumu, inatakiwa tucheze kimkakati, tunakwenda kucheza na timu ambayo ni nzuri ikicheza kwao. Ni hatari mno inapocheza uwanja wao wa nyumbani na hata mechi zote ilizoshinda ilicheza hapo.

Tunatakiwa kucheza kwa umakini, tunatakiwa tuwe waangalifu, tukiwa na mpira na kipindi ambacho hatuna, kwa maana hiyo tunakwenda kucheza kimkakati, nia ni moja tu tusipoteze mchezo, tushinde au tupate sare, kwa sababu wanapenda zaidi kushambulia, wanafunguka na ndiyo maana inafunga mabao mengi. Lakini sisi hatuingii kwenye mtego huo, hatuwezi kufunguka kama wao wanavyocheza na kupishana nao, ila hatutowapa nafasi ya kuumiliki mpira, na tutatumia nafasi ambazo wao wanaziacha kuwashambulia," alisema Fadlu.

Kocha wa Bravos do Maquis, Mario Soares, amewaonya wachezaji wake kuwa makini kwenye mchezo huo, kwani wapinzani wao wana wachezaji ambao wana uwezo wa kuimaliza mechi.

"Inawachezaji wazuri, ni ngumu kumtaja kila mmoja kwa jina, ila mmoja wao ni yule mwenye jezi namba 10 (Jean Ahoua), kwangu huyo ndiyo hatari zaidi, anacheza taratibu tu, lakini mipira yake ni hatari sana," alisema kocha huyo.

Simba yenye pointi tisa, inahitaji angalau sare ili kuweza kutinga hatua ya robo fainali, huku Bravos do Maquis ambayo ina pointi sita, inahitaji ushindi ili ifikishe pointi tisa, halafu isubiri mchezo wa mwisho ugenini dhidi ya CS Sfaxien ya Tunisia.