WAKATI mechi ya watani wa jadi nchini inatarajiwa kuchezwa kesho kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, nguvu ya Simba ipo katika mipira ya kona na matumizi mazuri ya vichwa huku Yanga ambao ni wenyeji wa dabi hiyo inaonekana hatari zaidi ikiingia ndani ya eneo la hatari.
Kwa mujibu wa takwimu za dawati la Nipashe zilizokusanywa kabla ya mchezo huo ambao huvuta hisia za mashabiki wa soka wa ndani na nje ya nchi, timu zote mbili zina maeneo ambayo ndiko inategemea kutumia kupata ushindi.
Takwimu zinaonyesha Simba ina mabao matatu yaliyotokana na mipira ya kona, huku Yanga ikiwa haina hata bao moja lililotokana na njia hiyo.
Simba ina mabao matano yaliyofungwa kwa vichwa, wakati Yanga ikiwa imepachika magoli manne kwa njia hiyo, huku timu zote mbili zikifanana kwa kila moja kufunga kwa mipira ya faulo moja ya moja kwa moja, na moja iliyosababishwa na mpira wa faulo.
Takwimu nyingine ambazo timu hizo inafanana ni kila upande umefunga mabao 14 kupitia upande wa kulia.
Kwa upande wa Yanga, takwimu zinaonyesha imefunga mabao 35 yaliyotoka na kutengenezwa na viungo kupitia katikati ya uwanja ambapo inaonekana eneo hilo ni hatari zaidi, huku upande wa kushoto ukizaliwa magoli matatu pekee.
Yanga inaonekana hatari wachezaji wake wakiingia ndani ya boksi, kwa sababu takwimu zinaonyesha mabao yake 41 yamefungwa ndani ya eneo hilo, huku mengine 11 yakifungwa nje ya boksi.
Takwimu pia zinaonyesha mabingwa hao watetezi, Yanga imefunga mabao 28 wachezaji wake wakitumia mguu wa kulia, na ya mguu wa kushoto wakiwa ni magoli 20, manne yakiwa ya vichwa.
Yanga inayofundishwa na Kocha Mkuu Miguel Gamondi, haijafunga bao lolote kwa kona, lakini imefunga magoli mawili kwa penalti na mabao manane yamepatikana kwa njia ya krosi.
Kwa upande wa Wekundu wa Msimbazi, mabao yaliyopitia katikati ya uwanja, yakitengenezwa na viungo wake ni 22, ikiwa ni pungufu kwa watani zao, na kufunga mabao nanne kupitia upande wa kushoto, ikiizidi Yanga goli moja.
Imefunga mabao 35 ndani ya boksi, matano nje ya boksi, takwimu ambazo ni chini ya zile za Yanga.
Simba inaonekana ina mabao mengi iliyofungwa mguu wa kulia, ikifanya hivyo mara 29 na kuizidi Yanga bao moja, lakini haina matumizi mazuri na mguu wa kushoto kwa wachezaji wake, wamefunga mabao sita tu wakati wenzao wana mabao 20.
Simba inaonekana ni hatari katika kutengeneza penalti, imefunga mabao saba ya mikwaju hiyo mpaka sasa, matano zaidi ya wapinzani wao, ikifunga mabao matano ya vichwa, ya kona matatu, huku ikipata mabao saba yaliyotokana na mipira ya krosi.
Yanga ambao ndio vinara wamecheza mechi 21 wakiwa na pointi 55 kibindoni wakati Simba yenye pointi 46 na iliyoko katika nafasi ya tatu kwenye msimamo imecheza michezo 20 ya ligi hiyo ya juu Tanzania Bara.
JKT Tanzania yenye pointi 22 sawa na Mashujaa FC pamoja na Tabora United, Mtibwa Sugar yenye pointi 17, ndio timu zilizoko mkiani katika msimamo wa ligi hiyo yenye timu 16.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED