TIMU ya Taifa ya Wasichana ya umri chini ya miaka 17 (Serengeti Girls), inatarajia kukutana na yosso wenzao wa Morocco katika mechi ya mashindano ya UNAF itakayochezwa leo jijini Tunis nchini, Tunisia.
Serengeti Girls ambayo ni nchi mwalikwa katika mashindano hayo ilianza kwa ushindi mnono wa mabao 4-1 dhidi ya Misri.
Akizungumza na gazeti hili jana, Kocha Mkuu wa Serengeti Girls, Bakari Shime, alianza kwa kuwapongeza wachezaji wake kwa kiwango kizuri walichokionesha kwenye mechi ya kwanza na anatarajia wataendelea kuimarika.
Shime alisema ameendelea kukijenga kikosi chake kwa sababu malengo yake ni kurejea nyumbani na ubingwa wa mashindano hayo.
Kocha huyo alisema mashindano hayo ni muhimu na yanawasaidia wachezaji wake kujijenga kisaikolojia na kuwapa uzoefu wa michezo ya kimataifa.
"Ninawapongeza sana wachezaji wangu kwa kiwango walichokionyesha katika mchezo wetu dhidi ya Egypt (Misri), haya mashindano ya UNAF ni makubwa na yanasaidia kuwajenga wachezaji wetu ambao wengi ni chipukizi na tunatumia kuwaandaa na michuano mingine iliyoko mbele yetu," alisema Shime.
Aliongeza siri ya kupata ushindi mnono katika mechi ya kwanza ni wachezaji wake kufuata maelekezo na kuwakumbusha kuwa watulivu wanapokaribia goli la wapinzani.
"Ingawa hatujapata muda mrefu wa kufanya maandalizi kwa ajili ya kushiriki mashindano haya, tunashukuru tumeanza vizuri, wachezaji wamecheza wakati wa jua kali, nyasi zilikuwa zinachoma lakini wamepambana na kupata magoli manne," alisema Shime.
Kocha huyo pia aliwashukuru Watanzania waliopo Tunisia kwa ushirikiano waliowaonyesha katika mchezo huo kwa kujitokeza uwanjani kuishangilia timu yao.
Serengeti Girls itashuka tena dimbani kesho kuvaana na wenyeji Tunisia.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED