TIMU ya Taifa ya Soka ya Tanzania chini ya miaka 17, Serengeti Boys imefanikiwa kufuzu kucheza fainali za Mataifa ya Afrika kwa umri huo zinazotarajiwa kuchezwa mwakani nchini Morocco baada ya kuifumua Sudan Kusini mabao 4-0 katika mchezo wa nusu fainali ya kusaka tiketi hiyo kwa ukanda wa CECAFA, uliochezwa jana mchana, Uwanja wa Nakivubo, Kampala, Uganda.
Mbali na kukata tiketi, Serengeti Boys pia imetinga hatua ya fainali ya michuano hiyo.
Mabao ya Serengeti Boys yalifungwa na Hussein Mbegu, Abel Joasiah na Ng'habi Zamu.
Kocha Mkuu wa timu hiyo, Agrrey Morris, ameelezea kufurahishwa kwake kuipeleka timu hiyo fainali, akisema hii ni mara ya kwanza kwenye historia yake ya soka.
"Namshukuru Mungu, Watanzania wote, hili ni jambo kubwa sana kwangu kwa sababu ni mara ya kwanza kwenye historia yangu ya soka kuiwezesha timu ya Tanzania kufuzu, nimefurahi sana, ni jambo zuri kwangu, sasa naangalia mbele hatujajua tunacheza na nani fainali, lakini yoyote yule aje," alisema.
Akuzungumzia mchezo huo alisema kuwa ulikuwa ni wa kimbinu zaidi na ndicho kilichofanya wapate ushindi huo.
"Ulikuwa ni mchezo wa kimbinu zaidi, tulisoma ubora na udhaifu wao na tukajua jinsi gani ya kukabiliana nao, kwa sababu wanapenda sana kushambulia, tukaweka wachezaji wawili wenye spidi ili tukitoka kwetu tuondoke kwa kasi na hii imetusaidia sana," alisema.
Alisema kwa sasa wanasubiri mchezo wa fainali kati ya wenyeji Uganda dhidi ua Somalia, akisema utakuwa mgumu na wenye mahitaji tofauti.
"Kila timu ina aina yake ya mchezo, kwa hiyo tunataka kuangalia ni timu gani itaingia fainali ili tujue namna ya kukabiliana nayo," alisema.
Uganda na Somalia pia zilitarajia kucheza jana katika mchezo wa pili wa nusu fainali.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED