Nkane awindwa na Mashujaa

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 06:04 AM Jun 16 2024
 Denis Nkane.
Picha: Yanga SC
Denis Nkane.

KLABU ya Mashujaa FC inamuwinda winga wa Yanga, Denis Nkane, ambaye wanaona anaweza kukiongeza nguvu kikosi chao kwa ajili ya Ligi Kuu Tanzania Bara msimu ujao.

Habari kutoka ndani ya klabu hiyo zinasema kuwa tayari wameanza mazungumzo na mchezaji huyo ambaye amekuwa hapati nafasi ya kucheza kwenye kikosi cha Mabingwa wa Tanzania Bara.

"Tunaongea na Nkane, siyo mchezaji mbaya, ana kipaji, ni winga mzuri, ana mbio, siyo mvivu, ni kwa vile Yanga kuna wachezaji wengi wenye ubora wa hali ya juu na yeye hachezi mara kwa mara, kama anakuja kwetu ambako atacheza mechi nyingi atarudi kwenye ubora wa hali ya juu, inawezekana kuliko alivyokuwa mwanzo wakati anatoka Biashara United kujiunga na Yanga," alisema mtoa taarifa ndani ya klabu hiyo.

Mchezaji huyo anayecheza winga ya kushoto, alijiunga na Yanga, 2022, akitokea klabu Biashara United, lakini kipindi chote hicho amekuwa na changamoto ya kupata namba kwenye kikosi cha kwanza, na kuna wakati akaandamwa na majeraha.

Mtoa taarifa huyo alisema maandalizi yote ya msimu ujao yanaelekea kukamilika likiwemo suala la usajili na Juni 28, wanatarajia kwenda Zanzibar kwa ajili ya kupiga kambi kwa ajili ya maandalizi ya Ligi Kuu msimu wa 2024/25.

"Tarehe 28 mwezi huu tunategemea kuanza maandalizi ya msimu ujao 'pre-season', tutafranyia maandalizi yetu Zanzibar.

Kuhusu maboresho, mwalimu ameshatoa ripoti yake, tumeifanyia kazi, tumeongeza baadhi ya wachezaji, tutawatangaza rasmi majina yao tutakapokuwa tayari kufanya hivyo. Kwa kikosi cha msimu ujao malengo yetu ni nafasi nne za juu," alisema.

Mashujaa, yenye maskani yake Mkoani Kigoma,  ilimaliza ligi msimu uliomalizika ikiwa kwenye nafasi ya nane ikicheza mechi 30, imeshinda mechi tisa, sare nane na ikapoteza mechi 13 na kukusanya pointi 35.