NCAA yaonya upotoshaji wanaohama Ngorongoro

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 10:20 AM Jun 25 2024
NCAA yaonya upotoshaji wanaohama Ngorongoro.
Picha: Mtandao
NCAA yaonya upotoshaji wanaohama Ngorongoro.

MAMLAKA ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro (NCAA) imezitaka baadhi ya taasisi na mashirika yasiyo ya kiserikali kutoka ndani na nje ya nchi kuacha upotoshaji kuhusu wananchi wanaohama kwa hiyari ndani ya hifadhi hiyo.

Wananchi hao ni wale wanaojiandikisha kwenda Kijiji cha Msomera, NCAA imewataka wapotoshaji wa mchakato huo kutafuta ukweli kuhusu suala hilo.

Akizungumza baada ya kumalizika kwa tamasha la jamii ya Wamasai lililofanyika ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro, Kaimu Meneja wa Uhusiano kwa Umma wa Mamlaka hiyo, Hamis Dambaya, amesema baadhi ya taasisi zimekuwa zikiripoti kabila la Wamasai wanaoishi ndani ya hifadhi hiyo wanafukuzwa na kuondolewa kwa nguvu.

Amekanusha upotoshaji huo na kueleza kwamba, ndio maana hata tamasha hilo limefanyika ndani ya Kreta ya Ngorongoro na kuhudhuriwa na watu mbalimbali wakiwamo watumishi.

Amesema jamii ya Kimasai, Wahadzabe, Wamang’ati wanaoishi ndani ya hifadhi imekuwa na ushirikiano mkubwa na Mamlaka hiyo ndiyo maana uelimishaji wa wananchi kuhama kwa hiyari umekuwa ukifanyika bila upinzani wowote.

Dambaya amesema katika tamasha hilo mamlaka hiyo imeelimisha wananchi kuhusu huduma za kijamii ambazo serikali inazitoa katika Kijiji cha Msomera kulinganisha na maisha ya ndani ya hifadhi na baadhi yao kueleza kuwa wapo tayari kuwafuata wenzao.