Watu wenye ulemavu waomba mil.13/- kufuga samaki

By Elizabeth John , Nipashe
Published at 07:01 AM Jun 26 2024
Shilingi Elfu kumi.
Picha: Mtandao
Shilingi Elfu kumi.

SERIKALI wilayani Wanging'ombe mkoani Njombe, imeombwa kusaidia kikundi cha Manange cha watu wenye ulemavu wa viungo na uoni hafifu Sh. milioni 13, ili kufanikisha kuchimba mabwawa ya samaki sita na kupata vifaranga kwa lengo la kujikwamua na umaskini.

Ombi hilo limetolewa na wanakikundi hao katika Kijiji cha Itambo wilayani humo wakati wakizungumza na waandishi wa habari.

Walisema wanaiomba serikali kuwasaidia kupata mkopo ili kujenga mabwawa sita ambayo wanaamini yatawasaidia katika kujikwamua kiuchumi.

“Tungefanikiwa kupata haya mabwawa sita tutashukuru sana serikali yetu, hata wakitupa mkopo sisi tutarejesha vizuri na hitaji letu ni Sh. milioni 13,” alisema Grayson Mkongwa.

Naye Stanely Mkongwa alisema tatizo kubwa ni kwamba wao hawana fedha ya kuwezesha kupata mabwawa na vifaranga vya samaki ili kuvipanda na baadaye wapate kipato kikubwa.

Aidha, alitoa rai kwa watu wenye ulemavu wilayani humo kufanya kazi kwa bidii badala ya kukaa nyumbani na kutegemea misaada kutoka kwa wadau jambo ambalo sio zuri.

Naye Ofisa Maendeleo ya Jamii Halmashauri ya Wilaya ya Wanging'ombe, Husna Lumaliza, aliwataka wanakikundi hao kutumia fursa ya kupata mikopo ya halmashauri ambayo itaanza kutolewa Julai mwaka huu.

Alisema mifumo ya utolewaji mikopo imewekwa vizuri kuwa ya kisasa tofauti na zamani.

Mwakilishi kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamiii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Grace Mbwilo, aliitaka Halmashauri ya Wilaya ya Wanging'ombe kuwawezesha watu wenye ulemavu na wengine waliopo kwenye vikundi kwa kuwapatia fedha za mikopo ili kufanikisha shughuli zao kiuchumi ambazo wanazifanya.