Serikali yasitisha ukaguzi risiti za EFD

By Paul Mabeja ,, Romana Mallya ,, Elizabeth Zaya , Nipashe
Published at 08:46 AM Jun 25 2024
Mgomo wa wafanyabiashara wa Soko la Kariakoo ukiendelea.
Picha: Mpigapicha Wetu
Mgomo wa wafanyabiashara wa Soko la Kariakoo ukiendelea.

SERIKALI imesitisha ukaguzi wa risiti za kielektroniki na ritani za kodi iliyokuwa ikifanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kupitia mkoa wa kikodi Kariakoo na maduka kufunguliwa jana.

Baadhi ya wafanyabiashara waliozungumza na Nipashe Digital waliokutwa wameketi nje ya maduka yao walisema walilazimika kutii agizo la viongozi wao la kufunga biashara ili changamoto wanazotaka zitatuliwe.

Mmoja wa wafanyabiashara wadogo aliyejitambulisha kwa jina moja la Fortunatus, amesema wanaendelea na biashara, lakini kwa jana haikuwa nzuri kama ilivyo siku zote.

“Yaani ni bora wafanyabiashara wafungue maduka yao, kwa sababu imetuathiri na sisi, wanunuzi wengi hawajafika leo kwa sababu wamesikia kuna mgomo kwa hiyo na hata kwetu biashara ni ngumu, hatujazoea namna hii,” amesema.

Nipashe Digital imeshuhudia baadhi ya wafanyabiashara wakiuza bidhaa kwa kufungua na kufunga maduka yao wakihofia wasigundulike kukiuka taarifa waliyopewa na viongozi wao.

“Yaani hapa tunachofanya hasa kwa wateja wetu wakubwa ili tusiwapoteze, wakija, unafungua anaingia dukani halafu unafunga mlango huku biashara ikiendelea ndani...na tumefanya hivi sana, hivi unafikiri utafanyaje, mteja ametoka mbali, amelipa nauli yake halafu usimuuzie...haiwezekani, kikubwa uhakikishe geti haliko wazi,” amesema mmoja wa wafanyabiashara katika eneo hilo la Kariakoo.

Wengine waliolalamika kukumbwa na athari iliyotokana na mgomo huo ni wachuuzi wa bidhaa kama matunda, nyanya, mboga na mamalishe, kwamba kutokana na idadi ndogo ya wanunuzi, mauzo hayakuwa mazuri kwao.

Baadhi ya wanunuzi ambao walizungumza na Nipashe akiwamo mkazi wa Gongolamboto, Agnes Martin, amesema  ni vema serikali ikamalizana na changamoto za wafanyabiashara hao ili isiwe jambo la kujirudia kila wakati.

UKAGUZI WASITISHWA

Wakati mgomo huo ukishika kasi, mkoani Dodoma kikao kilichofanyika baina ya serikali na viongozi wa wafanyabiashara kilitaja mambo sita yaliyofikiwa ni uamuzi wa kusitisha ukaguzi wa risiti za kielektroniki na ritani za kodi iliyokuwa ikifanywa na TRA.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo, ndiye aliyetoa maazimio ya kikao hicho na kueleza kuwa utaratibu huo umesitishwa na unaandaliwa mzuri wa utekelezaji wa suala hilo.

Prof. Mkumbo alisema mwezi Julai, TRA itapitia upya mfumo wa nyaraka ili kupata ukadiriaji sahihi na operesheni za kamata kamata ambazo ilikuwa inafanya mamlaka hiyo zimesitishwa.

Alisema suala la ukokotoaji wa kodi ni la kisheria, hivyo serikali inaendelea kuliangalia.

Kadhalika alisema serikali imewahakikisha itaendelea kuwapanga machinga kama Rais Samia Suluhu Hassan alivyoagiza ili wasiingiliane na wenye maduka.

“Tumewaeleza kwamba, Muswada wa Sheria ya Fedha 2024 bado haujapitishwa na Bunge na kwa sasa wanaita makundi mbalimbali kutoa maoni, hivyo tumewataka nao wapeleke maoni yao ili yafanyiwe kazi kabla haujapitishwa,” alisema.

Prof. Mkumbo alitaja jambo lingine ni kuhusu kamati ya Waziri Mkuu ambayo iliibuka na changamoto 41 na  kati ya hizo, 35 zikihusu mambo ya utendaji na sita kuhusu sheria na sera, ambapo zote zinafanyiwa kazi.

Wengine waliohudhuria kikao hicho kilichoongozwa na Waziri wa Fedha, Dk. Mwigulu Nchemba ni taasisi zinazosimamia masuala ya wafanyabiashara na Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Ashatu Kijaji na viongozi wengine waandamizi wa serikali.

WABUNGE WAHOJI

Baadhi ya wabunge jana walihoji na kutaka kupata majibu kutoka serikalini kuhusu mgomo wa wafanyabiashara hao.

Mbunge wa Geita Vijijini (CCM), Joseph Musukuma, aliomba mwongozo bungeni kuhusu sakata hilo akitaka kauli ya serikali baada ya wafanyabiashara hao kufunga maduka eneo la Kariakoo.

“Mheshimiwa Naibu Spika kumekuwa na kipeperushi kinatembea mitandao kuanzia siku ya Ijumaa, Jumamosi, Jumapili kuwa Jumatatu (jana) wafanyabiashara watafunga maduka ambayo ni leo (jana) na tunapozungumza sasa hivi Kariakoo imefungwa hakufanyiki biashara”.

Aliomba kupata kauli ya serikali kulingana na kinachoendelea eneo la Kariakoo, akitoa mfano wa watu wanatoka vijijini wanaokwenda jijini Dar es Saalam kufuata mahitaji na kukuta maduka yamefungwa.

Alisema baadhi ya watu hao wengi wao hawana pesa za kujikimu ikiwamo kulala jijini Dar es Salaam kwa sababu walitarajia kupata huduma na kurudi mikoani mwao.

Musukuma alisema baadhi ya watu wameanza kuwaomba fedha wabunge, hivyo aliomba mwongozo wa Naibu Spika akitaja kufahamu nini kauli ya serikali kukuhusiana na wafanyabiashara waliofunga maduka hayo.

Akijibu mwongozo huo, Naibu Spika, Mussa Zungu, alisema tangu juzi na jana viongozi wa serikali na wafanyabiashara wamekutana na taarifa rasmi kuhusu suala hilo zitatolewa baada ya kikao hicho kumalizika.

“Mheshimiwa Musukuma juzi kwenye mchango wako ulizungumzia hoja hii na juzi na jana viongozi wa serikali na wafanyabiashara wamekuta, taarifa rasmi ya serikali tutaipata baada ya kikao hicho kumalizika,” alisisitiza Zungu.

Mwishoni mwa wiki kilisambaa kipeperushi chenye ujumbe wa kuhamasisha mgomo kufanyika kuanzia jana, kikieleza kwamba hakuna duka litakalofunguliwa eneo la Kariakoo na yeyote atakayeonekana amefungua atashughulikiwa.

Sehemu ya kipeperushi hicho kilisomeka: 

“Wafanyabiashara wote wa Kariakoo mnatakiwa kufunga biashara zenu zote yakiwamo maduka na ofisi. Chochote unachokifanya kuanzia Jumatatu Juni 24 bila ukomo hadi pale changamoto zetu zote za kibiashara zitakapotatuliwa.”