Morocco: Lazima tuifunge Guinea

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 09:52 AM Nov 18 2024
Taifa Stars
Picha: Mtandao
Taifa Stars

KOCHA Mkuu wa Timu ya Taifa, Taifa Stars, Hemed Suleiman 'Morocco', amesema ushindi wa mabao 2-0 walioupata dhidi ya Ethiopia juzi nchini Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, umewapa chachu na nguvu ya kushinda mchezo wao wa kesho dhidi ya Guinea, akiongeza kuwa hakuna kiswahili kingine tena zaidi ya kuichapa timu hiyo ili Tanzania ifuzu kucheza fainali za Mataifa ya Afrika, (AFCON) 2025.

Akizungumza baada ya kumalizika kwa mchezo huo uliopigwa Uwanja wa Des Martyrs uliopo Kinshasa, ambako Ethiopia waliamua kuchezea mechi yao ya nyumbani huko kutokana na viwanja vyao kushindwa kukidhi vigezo vilivyowekwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), Morocco, alisema hakuna muda wa kupoteza wala kufurahia matokeo hayo, badala yake wanajipanga kwa mchezo ujao dhidi ya Guinea ambao ndio utatoa hatima ya Tanzania kwenda nchini Morocco kwa ajili ya fainali hizo.

Sasa tunahitaji kushinda mechi ya mwisho, hakuna kiswahili kingine, ili tufuzu ni lazima tushinde, tunarudi kwenye uwanja wa mazoezi ili tujipange na yale mapungufu yaliyoonekana tuyarekebishe, tunajua mechi itakuwa ngumu sana, ila ushindi huu dhidi ya Ethiopia umetutia chachu, tutakuwa imara zaidi katika mchezo ujao kuliko huu," alisema kocha huyo.

Akizungumzia mazingira ya mchezo wenyewe, alisema haikuwa rahisi kutokana na falsafa ya mpira wa Ethiopia ambao mara zote ni kumiliki mpira, hivyo ilibidi wafanye kazi ya ziada.

"Tulijua kuwa mechi itakuwa ngumu kwa sababu Ethiopia ni timu ambayo inajua sana kumiliki mpira, ndiyo uchezaji wao, ndiyo falsafa yao ya miaka yote, mkakati tulioingia ni kuzuia njia zao na tulitaka kuimaliza mechi mapema, na iliwezekana kwani tulitengeneza nafasi nyingi hatukuzitumia, ni mbili tu ndiyo tulifanikiwa kufunga," alisema.

Naye mfungaji wa bao la kwanza, Simon Msuva, alisema wamefurahi kupata ushindi, lakini bado wana kazi kwani wanakwenda kucheza mchezo mgumu zaidi, lakini akiwatoa wasiwasi Watanzania kuwa watafanya kila linalowezekana kuweza kupata matokeo ya ushindi.

"Mechi ilikuwa nzuri, ilikuwa ngumu, lakini tumeshinda, tumefurahi ila kazi bado inaendelea kwa sababu tuna mchezo mwingine mgumu dhidi ya Guinea. Tunahitaji ushindi tu ili tufuzu, tunaomba Watanzania tuungane kwa pamoja, sisi ndani ya uwanja tutapambana kwa ajili yao," alisema.

Yalikuwa ni mabao ya Msuva na Feisal Salum 'Fei Toto' yaliyofanya Stars kufikisha pointi saba, ikihitaji kuifunga Guinea tu yenye ponti tisa, ili kufikisha pointi 10 na kufuzu AFCON kwa nafasi ya pili, baada ya DR Congo kuwa timu ya kwanza kwenye Kundi H kufuzu fainali hizo zitakazofanyika mwakani nchini Morocco.