UTT AMIS yajivunia thamani ya mifuko kuongezeka hadi tril. 2.2/-

By Frank Monyo , Nipashe
Published at 01:12 PM Nov 18 2024
MKURUGENZI Mtendaji wa UTT AMIS, Simon Migangala.
Picha:Mpigapicha Wetu
MKURUGENZI Mtendaji wa UTT AMIS, Simon Migangala.

MKURUGENZI Mtendaji wa UTT AMIS, Simon Migangala, amesema juhudi za kuboresha mifumo ya kidijitali, mazingira thabiti ya uwekezaji na utulivu wa soko, zimewezesha taasisi hiyo kupata mafanikio makubwa, thamani ya mifuko ikiongezeka hadi Sh. trilioni 2.2 kufikia Juni 30 mwaka huu kutoka Sh. trilioni 1.6 Juni 2023.

Alitoa kauli hiyo mwishoni mwa wiki wakati wa Mkutano Mkuu wa 16 wa Mfuko wa Umoja uliokutanisha wawekezaji wa mifuko ya taasisi hiyo ambayo ni Umoja Fund, Wekeza Maisha Fund, Watoto Fund, Jikimu Fund, Liquid Fund na Bond Fund.

"Mifuko yetu imefanya vizuri sana, ikikua kutoka Sh. trilioni 1.6 mwaka 2022/23 hadi Sh. trilioni 2.2 mwaka 2023/24, ikiwa na faida ya asilimia 12 au zaidi kwenye kila mfuko, kwa mujibu wa mpango huo wa uwekezaji wa pamoja.

"Tunawashukuru wawekezaji wetu kwa imani yao endelevu, pamoja na serikali. Tumejizatiti kuboresha mazingira ya uwekezaji nchini. Tunatarajia mafanikio makubwa zaidi," alisema Migangala.

Alisisitiza kuwa mkakati wa sasa wa UTT AMIS ni kuboresha miundombinu ya teknolojia ili kufikia watanzania wengi zaidi.

Aliongeza kuwa faida ya mwaka 2023/24 ni zaidi ya Sh. bilioni 250, akiitaja ni ongezeko kubwa kulinganishwa na mwaka uliopita. 

Mkurugenzi huyo alisema mpango huo wa uwekezaji wa pamoja umeweka lengo la kuongeza thamani ya mifuko hadi Sh. trilioni 2.5 ifikapo mwaka ujao wa fedha, akidokeza kuwa tayari wameona dalili za kufikiwa kwa lengo hilo kwa hesabu za miezi minne ya mwanzo kufikia mwezi Oktoba mwaka huu.

Alisema licha ya changamoto za kimataifa kama vile vita na taharuki ya kisiasa, uchumi wa Tanzania umeendelea kuimarika, ukirekodi ukuaji wa asilimia 5.1 mwaka 2023 na matarajio ya ukuaji wa asilimia 5.4 mwaka huu (2024). 

Mkurugenzi huyo alisema mfumuko wa bei ulibaki katika kiwango cha asilimia 3.1 chini ya matarajio ya asilimia 5.0. Ukuaji wa sekta ya mitaji pia ulionekana; bei za hisa ziliongezeka kwa asilimia 9.3 katika Soko la Hisa la Dar es Salaam.  

Migangala alikiri kuwa idadi ya watanzania wanaowekeza katika mifuko hiyo ni ndogo, kauli iliyoungwa mkono na Mwenyekiti wa Bodi ya UTT AMIS, Prof. Faustine Kamuzora, aliyesema, "licha ya mifuko ya uwekezaji kuwa na faida nyingi, kumekuwapo mwitikio mdogo wa wananchi kujiunga kutokana na kukosa elimu ya uwekezaji".

Aliongeza kuwa wakati watanzania wakiwa zaidi ya milioni 60 (Sensa ya Watu na Makazi 2022), waliowekeza katika mifuko hiyo hawazidi milioni moja, hivyo elimu zaidi inahitajika ili kufahamu umuhimu wake.

"Wananchi katika hili wanapaswa kujua kwamba usipokuwa na uwezo wa kutengeneza fedha wakati umelala, ni hatari kwako na badala yake ni lazima kila siku ukimbizane na biashara na kila senti unayoipata na wakati mwingine mambo yanaweza yasiwe mazuri kwako katika kukimbizana huko.

"Hivyo, unavyowekeza fedha katika mifuko kama hiyo, mtaji wako unaendeshwa na wataalamu ambao wanajua soko linavyokwenda na kukuzalishia faida kila uchwao," alisema.

Aliongeza kuwa katika kukabiliana na changamoto hiyo, UTT AMIS inatekeleza mikakati mbalimbali inayolenga kuongeza ujumuishi wa kifedha na kuvutia wawekezaji wengi zaidi.

"Mwaka huu umekuwa wa mafanikio makubwa kwa mifuko yetu kutokana na imani kwa wataalamu wetu. Mifuko ni salama na hatari zinazohusiana na uwekezaji ni ndogo. Watanzania wanaweza kuwa na uhakika wa kupata faida mwishoni mwa mwaka," alisema Prof. Kamuzora.