UCHAGUZI WA MITAA: CCM, CHADEMA 'weka, tuweke' miji ya kimkakati

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 12:41 PM Nov 18 2024
CCM, CHADEMA 'weka, tuweke' miji ya kimkakati
Picha: Nipashe Digital
CCM, CHADEMA 'weka, tuweke' miji ya kimkakati

ZIKIWA zimebaki siku nane kabla ya kufanyika kwa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, takwimu za awali kuhusu namna vyama vilivyosimamisha wagombea, zinaonesha kutakuwa na mchuano mkali kati ya CCM na CHADEMA katika miji inayotajwa kuwa ya kimkakati kisiasa.

Jijini Dodoma juzi, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI, Mohamed Mchengerwa alitoa taarifa kwa waandishi wa habari kuhusu mwenendo wa mchakato wa uchaguzi huo, ikionesha kuwa vyama vya upinzani vikiongozwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) vilijikita zaidi katika maeneo ya miji ya kimkakati kisiasa kusimamisha wagombea.

Ni mkakati unaolenga kujiimarisha kisiasa katika miji na majiji husika kuelekea Uchaguzi Mkuu mwakani, huku kukiwa na kumbukumbu ya CHADEMA kufanya vizuri katika miji hiyo wakati wa Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2015, ikishinda viti vya ubunge katika majimbo kama vile Mbeya Mjini, Musoma Mjini, Tarime Mjini, Bukoba Mjini, Arusha Mjini, Moshi Mjini, Ubungo, Kibamba na Ukonga. 

Katika ufafanuzi wake, Waziri Mchengerwa alisema kuwa kati ya nafasi 80,430 zinazogombewa, vyama 18 vya siasa vimeweka wagombea katika nafasi 30,977 sawa na asilimia 38.51, ukiacha Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambacho imeweka wagombea katika nafasi zote.

Kati yake, nafasi za mwenyekiti wa kijiji zinazogombewa ni 12,280, upinzani ukiweka wagombea katika nafasi 6,060 sawa na asilimia 49.35 ya nafasi hizo; mwenyekiti wa mtaa kuna nafasi 4,264 lakini upinzani umweka wagombea katika nafasi 3,281 sawa na asilimia 76.94 ya nafasi hizo.

Nafasi za mwenyekiti wa kitongoji zinazogombewa ni 63,886, lakini vyama 18 vya siasa vimeweka wagombea katika nafasi 21,636 sawa na asilimia 33.87 ya nafasi hizo.

MIJI YA KIMKAKATI

Waziri Mchengerwa alieleza namna mchuano ulivyo katika kusimamisha wagombea maeneo ya miji, akiweka wazi kuwa "huko ndiko kwenye maeneo ya kimkakati kisiasa".

Alisema Jiji la Mbeya lina mitaa 181, CCM walichukua fomu kwenye mitaa yote 181, CHADEMA walichukua fomu katika mitaa 154 na wameteuliwa kwenye mitaa 153; CUF walichukua fomu katika mitaa 154 na wameteuliwa wote, ACT Wazalendo walichukua fomu katika mitaa tisa na wameteuliwa wote, TLP walichukua fomu katika mtaa mmoja na mgombea wao huyo ameteuliwa.

Katika Jiji la Arusha, Waziri Mchengerwa alisema kuna mitaa 154, CCM walichukua fomu katika mitaa yote 154, lakini wagombea wao tisa hawakuteuliwa, waliwekewa pingamizi. CHADEMA walichukua fomu katika mitaa 154, waliorejesha ni 142 na walioteuliwa ni 95.

Alisema Jiji la Dodoma lina mitaa 222, CCM walichukua fomu kwa mitaa yote 222, CHADEMA walichukua fomu kuwania mitaa 81 na wameteuliwa 67.

Mchengerwa alisema kuwa katika Jiji la Mwanza, CCM walichukua fomu kuwania mitaa yote 175, CHADEMA walichukua fomu kuwania mitaa 160 na wameteuliwa 153.

Waziri huyo alisema kuwa Manispaa ya Temeke ina mitaa 142, CCM walichukua fomu kuwania mitaa yote 142. CHADEMA walichukua fomu kuwania mitaa 105, wameteuliwa 96.

Katika Halmashauri ya Manispaa ya Moshi yenye mitaa 60, CCM walichukua fomu za mitaa yote, CHADEMA walichukua fomu za mitaa 59 na wameteuliwa 46, CUF walichukua fomu mitaa miwili na wameteuliwa wote, ACT walichukua fomu 22 na wameteuliwa 16.

Alisema kuwa katika Halmashauri ya Manispaa ya Singida yenye mitaa 53, vijiji 19 na vitongoji 83. Katika maeneo hayo CCM walichukua fomu kuwania mitaa, vijiji na vitongoji vyote. CHADEMA walichukua fomu kuwania mitaa 23, vijiji sita na vitongoji 25 na wameteuliwa katika mitaa ni 19, vijiji sita na vitongoji 23.

Waziri Mchengerwa alisema kuwa katika Manispaa ya Iringa yenye mitaa 131, CCM walichukua fomu kwenye mitaa yote, CHADEMA walichukua fomu kuwania mitaa yote 131 na wameteuliwa 127.

Alisema Halmashauri ya Manispaa ya Kigamboni ina mitaa 67, CCM walichukua fomu kwa mitaa yote,  CHADEMA walichukua za mitaa 42 na wameteuliwa 40.

Alisema katika Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela ambayo ina mitaa 171, CCM walichukua fomu kwa mitaa yote, CHADEMA walichukua fomu katika mitaa 133 na wameteuliwa 132.

Halmashauri ya Mji wa Tarime ina mitaa 81, CCM walichukua fomu kwa mitaa yote, CHADEMA walichukua fomu za kuwani mitaa 79 na wameteuliwa 76. 

Mjini Bunda kuna mitaa 84, CCM walichukua fomu kwa mitaa yote, CHADEMA walichukua za mitaa 73 na wameteuliwa 70.

Katika Halmashauri ya Mji wa Mbulu yenye mitaa 58, CCM walichukua fomu kwenye mitaa yote, CHADEMA walichukua 39 na wameteuliwa.

Alisema Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi ina vijiji 101, CCM walichukua fomu kuwania vijiji vyote, CHADEMA walichukua fomu kutaka kuongozi vijiji 71 na wameteuliwa 67.

Alisema Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe ina vijiji 76, CCM walichukua fomu katika vijiji vyote, CHADEMA walichukua vijiji 76 na wakateuliwa 73, ACT walichukua vijiji 17 na wakateuliwa 17.

Pia alisema kuna vitongoji 513 ambapo CCM walichukua katika vitongoji vyote na kuteuliwa wote, CHADEMA walichukua 449 na wakateuliwa 443, ACT walichukua 11 na wameteuliwa 10. 

Alisema Halmashauri ya Wilaya ya Musoma Vijijini ina vijiji 88 na vitongoji 500. CCM walichukua fomu kwa vijiji na vitongoji vyote, huku CHADEMA wakichukua fomu katika vijiji 81 na wakateuliwa 78 na vitongoji 397 na wameteuliwa 359.

Hata hivyo, Waziri Mchengerwa alibainisha kuwa takwimu hizo ni kabla ya kukamilika kwa hatua ya rufani za uteuzi, hivyo takwimu sahihi za walioteuliwa zitatolewa baadaye.