MKURUGENZI Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Prof. Mohamed Janabi, amesema ulaji wa chakula cha kila siku ndio unaotafsiri afya ya sasa na baadae, na kwamba walio na umri kuanzia miaka 35 ama 0 na kuendelea kuwa makini na aina ya mlo.
“Binafsi huwa sinywi juisi iliyotengenezwa au iliyotokea viwandani ni takribani miaka 20 tangu mwaka 2000. Sichanganyi matunda, nakula asubuhi tunda moja labda ndizi, mchana peazi na usiku kipande cha papai,” ameongeza.
“Jamii ibadili mtazamo kwamba uwekezaji wa maisha ya baadae, unaegemea kwenye uwekezaji wa mali, bali hatua hiyo inahitajika kwenye afya pia.”
Prof. Janabi ambaye pia ni daktari bingwa wa magonjwa ya moyo, anayasema hayo kupitia ukurasa wake wa kijamii kuhusu maisha bora, ikiwa ni mwendelezo wa elimu kwa umma, kuepukana na magonjwa yasiyoambukiza (NCDs) kama vile kisukari, presha na saratani.
“Wengi kwenye jamii hujiandaa kwa maisha ya baadae au ya kustaafu kwa kuwekeza katika mali hasa kujenga nyumba, ili aje akae kwake na pazuri miaka ijayo. Katika afya pia tunahitaji kuwekeza, una miaka kuanzia 35 au 40 na kuendelea unahitaji kulinda afya na kuzingatia mtindo wa maisha.
“Ulaji wa maji, matunda uwe wa kiasi gani? Ni kati ya maswali ambayo yanaulizwa sana. Unywaji maji unategemeana na shughuli ya mtu na mtu. Kunywa maji kati ya lita moja hadi moja na nusu kwa siku. Mfano mimi binafsi mara nyingi huwa sinywi maji zaidi ya lita moja na nusu.
Lakini wewe uko pale ofisini kuna AC umekaa tu, maji lita tatu hadi nne! Kuwe na sababu umefanya kitu, mazoezi labda hasa kipindi kama cha Desemba kuna joto kali, kwa sababu umetembea umetoka jasho umepoteza maji,” anasema bingwa huyo.
Anasema unywaji wa maji usiozingatia uwiano wa mwili, shughuli inayofanywa na mtu huweza kusababisha maumivu ya kichwa kutokana na ku-dilute sana damu na kuleta ‘electrolyte imbalance’ mwilini na hata kuufanya moyo kwenda mbio.
“Maji ni ‘solvate’ kwenye miwili yetu kuna ‘potassium, minerals’ na kadhalika. Miili yetu pia kwa asilimia 90 ni zaidi maji, hewa na chakula. Mapigo ya moyo yako bilioni 4.5 hadi tano katika maisha yetu. Katika kila dakika lita tano za damu zinapita kwenye moyo.
Kunywa wastani wa lita moja au 1.5 kwa siku, tembea hatua 10,000, epuka vyakula vya sukari, mafuta, kula mboga za majani na matunda katika kila mlo.
“Urefu wa afya inaathiri maisha yetu. Inakadiriwa ifikapo mwaka 2035 wengi watapoteza maisha duniani kutokana na mlo kuwasababishia NCDs. Watu milioni 35 kwa mwaka hufa kwa mwaka kutokana magonjwa ambayo hayasababishwi na bakteria bali kutokana na wanga. Binafsi nakula mlo mmoja, kwa miaka miwili sasa,” anasema.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED