MAAFANDE wa KVZ FC, wamejikuta wakibanwa mbavu na Wanamaji KMKM SC kwa kutoka sare tasa katika mechi ya mwendelezo wa Ligi Kuu Zanzibar mzunguko wa 11.
Mchezo huo ulichezwa juzi Jumamosi katika dimba la Mau A majira ya saa kumi alasiri na kuhudhuriwa na mashabiki kiasi wa timu zote mbili.
Akizungumza na gazeti hili juzi Kocha wa KMKM SC, Ame Msimu, alisema licha ya kutotarajia matokeo hayo ya sare, lakini tangu hapo awali alijua mchezo huo utakuwa mgumu.
Alisema kipindi cha kwanza timu yake ilicheza vizuri, lakini walishindwa kupata bao licha ya kutengeneza nafasi nyingi.
Msimu alisema wapinzani wao walikuwa bora katika kipindi cha pili ambacho walimiliki mpira na kuwashambulia, lakini umakini wa safu yake ya ulinzi uliweza kuhimili mashambulizi hayo.
“Ulikuwa mchezo mgumu sana, kwa kuwa kila timu ilishuka uwanjani lengo likiwa ni kupata alama ambazo zitamweka juu, lakini haikuwa bahati na tumegawana alama,” alisema.
Aidha, alisema kuwa bado timu yake inahitaji kupata ushindi wa alama tatu kutokana na matokeo ya michezo iliyopita ya kupata sare na kufungwa.
Alisema anaenda katika uwanja wa mazoezi kwa kuyafanyia kazi makosa ambayo mara kwa mara yanajitokeza katika timu yake.
Hata hivyo, aliwataka mashabiki wa timu hiyo kuendelea kutoa hamasa kwa timu yao ili kuwapa moyo wachezaji wao hasa katika wakati huu ambao hawana mlolongo mzuri wa matokeo.
Kwa matokeo hayo KMKM SC imekwea nafasi moja juu ikitokea ya saba hadi ya sita na alama zake 17 wakati Maafande wa KVZ FC wakiwa nafasi ya tano na alama zao 18.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED