Fadlu apagawa kipaji cha Mpanzu, awaita mashabiki

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 10:14 AM Nov 18 2024
Kocha Mkuu wa Simba, Fadlu Davids.
Picha: Simba SC
Kocha Mkuu wa Simba, Fadlu Davids.

WAKATI dirisha dogo la usajili likikaribia kufunguliwa Desemba 15, mwaka huu, Kocha Mkuu wa Simba, Fadlu Davids, amewaambia wanachama na mashabiki wa Simba kuwa, wakae tayari kumuona mchezaji mpya, Elie Mpanzu, akisema ataongeza kitu ndani ya kikosi chake kutokana na kipaji kikubwa alichonacho, huku akimtabiria makubwa.

Kocha huyo raia wa Afrika Kusini, alisema jana kuwa anaamini kutokana na kipaji alichonacho, atafunga mabao mengi na kuwasaidia wenzake kuwapa pasi za mwisho kwa ajili ya kupambania nembo ya klabu hiyo.

Ijumaa iliyopita, mchezaji huyo alicheza kwa dakika kadhaa kwenye mchezo wa kirafiki dhidi ya KMC, uliochezwa Uwanja wa KMC Complex, Mwenge, Dar es Salaam na kutoka sare ya bao 1-1, lakini haikuhudhuriwa na mashabiki.

"Tunategemea kuwa atafunga sana na atatengeneza nafasi nyingi kwa wenzake, tunategemea atafiti kwenye kila mfumo wetu, tunamtegemea sana Mpanzu kuleta upinzani ndani ya kikosi," alisema kocha huyo.

Mpanzu ataanza kuitumikia Simba kwenye mashindano rasmi Desemba 15 wakati timu hiyo itakapocheza mechi yake ya raundi ya tatu ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya CS Sfaxien ya Tunisia, utakaopigwa, Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, huku akitarajiwa kuonekana kwa mara ya kwanza kwenye Ligi Kuu itapovaana na KenGold, Desemba 18, Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam.

"Mpanzu ni mchezaji wa kipekee sana, tumekaa naye vikao vingi kuona ni sehemu gani anaweza kuzoea na kuwa huru akicheza uwanjani, tunataka azoee mipango yetu ajue nini cha kufanya akiwa na mpira, nafasi ipi achukue uwanjani akiwa na mpira na hata asipokuwa nao.

"Tumekaa naye vikao kuangalia ni namna gani anaweza kushambulia kulingana na wapinzani wetu wanavyocheza, nini tunafanya tunapokuwa tuna mpira, muda ambao hatuna, kinachobaki ni yeye mwenyewe kujiweka sawa na kuzoea mifumo yetu kwa kuwa bado hajaanza kucheza michezo ya mashindano, ila hii michezo ya kirafiki itamsaidia," alisema kocha huyo.

Mabosi wa Simba walimpa mkataba winga huyo raia wa Jamhuri ya Kidemkorasi ya Congo, kabla ya dirisha dogo la usajili.

Awali, Mpanzu, alikuwa asajiliwe na Simba kipindi cha dirisha kubwa, lakini dili liliharibika baada ya kutimkia nchini Ubelgiji kwenda kufanya majaribio katika Klabu ya Genk, ambayo hayakufanikiwa.

Baada ya kutofanikiwa na kumaliza mkataba wake na AS Vita, Simba ilirejea kwenye meza ya mazungumzo na mchezaji huyo, ikampa mkataba haraka kabla ya dirisha dogo ili kuepuka dili hilo kuvunjika tena.