Makamu wa Rais awapa majukumu matatu mawaziri wa biashara Afrika

By Rahma Suleiman , Nipashe
Published at 07:06 AM Jun 26 2024
Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Hemed Suleiman Abdullah.
Picha: Mtandao
Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Hemed Suleiman Abdullah.

MAKAMU wa Pili wa Rais Zanzibar, Hemed Suleiman Abdullah, amewataka mawaziri wa biashara Afrika kuweka mikakati imara itakayosaidia kuunganisha Afrika, kukuza biashara za ndani.

Aliyasema hayo jana visiwani Zanzibar wakati akifungua mkutano wa 14 wa mawaziri wa biashara wa eneo huru la biashara Afrika.

Alisema kuwapo kwa eneo huru la biashara ni hatua muhimu ya mwelekeo sahihi katika kutimiza ndoto za viongozi ambao walipigania ili kuhakikisha Afrika inajitegemea kiuchumi.

Hemed alisema Afrika inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwamo kukosekana kwa usalama wa baadhi ya maeneo, ukosefu wa nishati ya kutosha, miundombinu ya barabara, reli na usafiri wa anga, uzalishaji mdogo pamoja changamoto ya mawasiliano kutokana na kuwapo kwa lugha nyingi miongoni wa wananchi.

Aidha, alisema eneo lingine la kujikita ni kuwezesha biashara ndogo na za kati zishiriki kikamilifu katika biashara za kikanda na kimataifa pamoja na kuhakikisha upatikanaji wa mikopo nafuu, elimu ya biashara na makosa.

Alisema pia kuhakikisha ushirikiano wa kikanda ambao ni muhimu kwa mafanikio ya eneo huru la biashara la Afrika, kupunguza urasimu, kuimarisha utawala bora, kuhakikisha usalama wa mitaji na mali za wawekezaji ambapo kufanya hivyo kutasaidia kuvuta wawekezaji.

Hata hivyo, alisema Jamhuri ya Muunano wa Tanzania iko tayari kushirikiana na nchi zote wanachama wa eneo huru la biashara la Afrika katika kufanikisha malengo yaliyowekwa.

Waziri wa Biashara na Viwanda, Omar Said Shabani alisema, wamejadiliana na masuala muhimu katika biashara Afrika ikiwamo mabadiliko ya hali ya hewa na mapinduzi ya kijani ya maendeleo ya viwanda.

Aidha, alisema wamezungumzia fursa zilizopo katika uzalishaji wa vipuri vya magari ili kunufaika na biashara katika sekta ya magari ambayo ni sekta inayokuwa kwa kasi.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Kazi na Uwekezaji, Shari Ali Saharif, alisema Rais Dk. Samia Suluhu na Dk. Hussein Ali Mwinyi ni viongozi mashuhuri na shupavu.

Alisema pia ni watetezi wa dhati wa ushirikiano wa kiuchumi na maendeleo kote Afrika.