Mzize atamani kuifunga Simba

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 06:35 AM Apr 17 2024
news
Picha: Maktaba
Straika wa Yanga, Clement Mzize.

STRAIKA wa Yanga, Clement Mzize amesema kiu yake ni kufunga bao katika mechi ya Jumamosi dhidi ya Simba.

Mzize ambaye katika mechi ya Jumapili iliyopita alitoa pasi mbili za mabao, Yanga ikishinda mabao 3-0 dhidi ya Singida Fountain Gate, Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza, alisema baada ya kutoa 'asisti' mbili katika mechi hiyo, sasa anatamani kutupia katika mechi ya 'dabi', itakayochezwa Uwanja wa Benjamin Mkapa Jumamosi.

Straika huyo anaamini kuwa mchezaji anapofunga katika mechi ya 'dabi' basi rekodi inaendelea kubaki na kukumbukwa kwenye historia ya soka la Tanzania, pamoja na rekodi za michezo hiyo ya watani.

"Nimetumwa na wachezaji wenzangu, wameniambia niwaambie mashabiki wajae kwa wingi uwanjani ili tuwafurahishe, tusipowaona wao mioyo yetu inafifia, lakini tukiona wamejaa na wanatushangilia na sisi tunakuwa na morali ya hali ya juu sana.

"Naamini katika mechi ya Jumamosi tutapata ushindi, nakumbuka katika mechi dhidi ya Simba iliyopita 'niliasisti' mara mbili kama hii ya Singida Fountain Gate, sasa kwenye mechi hii naweza kufunga kabisa, natamani iwe hivyo ili kuzidi kuwafurahisha wanachama na mashabiki wa Yanga," alisema Mzize.

Katika mechi dhidi ya Singida Fountain Gate, Mzize alitoa pasi za mwisho zilizozaa mabao mawili, la pili na la tatu kwenye mchezo huo kwa Stephane Aziz Ki dakika ya 65 na Joseph Guede, dakika ya 67.

Katika mechi ya watani iliyopita ambayo ilichezwa Novemba 5, mwaka jana, alitoa 'asisti' mbili, moja kwa Aziz Ki, aliyefunga bao dakika ya 73 na nyingine kwa Maxi Nzengeli, akipachika bao dakika ya 77, na kuisaidia timu yake ya Yanga kupata ushindi wa mabao 5-1, mechi ikipigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Wakati Mzize akisema hayo, Kocha Mkuu wa timu hiyo, Miguel Gamondi amesema anakitayarisha kikosi chake kwa ajili ya kupambana na timu ngumu ya Simba katika mechi ya watani wa jadi na si vinginevyo.

Alisema hawezi kusema kwamba wanaweza kushinda idadi ya mabao kama waliyoshinda mechi ya mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

"Huwezi kusema utashinda mabao mengi au kama yale kwa sababu hata siku ile hakuna aliyetarajia kushinda idadi ile ya mabao, huu ni mpira na hii ni dabi, mimi nimeandaa kikosi changu kwa ajili ya kucheza mechi hiyo ili kushinda na kuwafurahisha mashabiki wetu, mengine huwa yanatokea hapo hapo uwanjani," alisema kocha huyo.

Yanga inakwenda kucheza mechi hiyo ikiwa imetoka kuibugiza Singida Fountain Gate mabao 3-0, huku watani zao wa jadi wakiwa na vikao vingi vinavyotokana na kutofanya vema kwenye michuano mbalimbali, Ligi ya Mabingwa Afrika, Kombe la FA na Ligi Kuu Tanzania Bara.

Mabingwa hao watetezi, wanaongoza ligi wakiwa na pointi 55, ikicheza mechi 21, kushinda 18, sare moja na kupoteza mbili, ikiwa imeshapachika mabao 52 mpaka sasa.